Naibu Waziri SELEMAN JAFO aagiza Wazazi Wasiopeleka watoto Shule Wawajibishwe
Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Selemani Jafo akitoka kukagua ujenzi wa choo cha walimu
katika shule ya msingi Chang’ombe ‘B’ wakati
wa ziara yake aliyoifanya katika kata ya Chang’ombe manispaa ya Dodoma.
Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Selemani Jafo akizungumza mara baada ya kumalizia ziara yake
kwa kukagua miundo mbinu ya majitaka katika shule ya msingi Chadulu na kutoa
maagizo kwa wakuu wa wilaya nchini.
................................................
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo amewaagiza Wakuu wa wilaya
nchini kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza
mwaka huu wanakwenda kuanza shule huku akiwasisitiza wazazi watakaoshindwa
kuwapeleka shule watoto hao wachukuliwe hatua za kisheria.
Jafo ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara ya
kukagua miundombinu mbalimbali katika shule za msingi, Chadulu, Chang’ombe A na
B, Manispaa ya Dodoma.
Katika ziara yake ya kukagua maagizo
aliyoyatoa kwenye shule hizo kuhusu masuala ya miundombinu, Jafo amesema “Sisi
kama serikali hatutaki mtoto akose elimu hasa katika kipindi hichi ambacho
serikali imeamua kuelekeza nguvu za kutosha kwenye elimu kwa ajili ya
watanzania.”
Ameongeza “Kwa mzazi ambaye mtoto wake
atabainika hajaenda shule na kupewa kazi zingine kama kuendesha bodaboda hatua
za kisheria zichukuliwe mara moja,”.
Pamoja na hayo, Jafo amekemea tabia ya
wazazi kutotilia mkazo masuala ya elimu na kuwakabidhi watoto wao kuendesha
bodaboda kama ajira yao badala ya kuwapeleka shule na kuwataka kuhakikisha
wanawanunulia mahitaji yote ya shule.
Aidha amesema serikali haitarajii kuna vijana
waliochaguliwa wakishawishiwa na wazazi kufanya vibaya kwenye mitihani kutokana
na elimu kuwa ni bure.
Akizungumzia kuhusu watoto walioandikishwa
kuanza kusoma elimu ya awali na msingi, Jafo amesema kumekuwepo na mwitikio
mkubwa katika suala la uandikishaji watoto hao na linatokana na uwepo wa elimu
bure.
Hata hivyo, amesema shule nyingi idadi ya
wanafunzi imeongezeka zaidi na kwa serikali ni faraja kuona watanzania wengi
sasa wanapata elimu huku akiwataka wazazi wahakikishe watoto walioandikishwa
wanahudhuria shule ipasavyo na wakurugenzi kuendelea kuweka mazingira
bora ya kujifunzia na kufundishia.
Kadhalika, Jafo ameridhishwa na ukarabati wa
miundombinu mbalimbali kwenye shule hizo huku akiwaahidi walimu kuwa serikali
itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia ili waweze kufanya kazi zao kwa
ufanisi.
Naye, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin
Kunambi, amesema kwasasa Manispaa hiyo inaendelea kukabiliana na changamoto
mbalimbali ikiwa ni pamoja ujenzi wa shule za msingi na sekondari na kuongeza
madarasa kwenye baadhi ya shule ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi hasa wanaohamia
Dodoma.
Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)
Seleman Jafo akipokea taarifa za maendeleo ya ujenzi wa madarasa shule ya msingi Chang’ombe ‘A’
kutoka kwa Afisa mteule daraja la -I- ambaye ni Fundi mkuu kutoka (JKT) Aluleyani
Mapunda wakati alipofanya
ziara ya kukagua
ujenzi wa madarasa shule ya msingi hiyo unaofanywa katika kata ya Chang’ombe mjini Dodoma.
Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Selemani Jafo
akipokea
maelekezo kutoka
kwa Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi juu ya
ukamilishaji ujenzi wa choo cha
walimu shule ya msingi Chang’ombe ‘B’ pia uendelevu wa ujenzi wa vyoo
vya wanafunzi katika ziara yake aliyoifanya katika kata ya Chang’ombe.
Post a Comment