Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi
(katikati) akipata taarifa kutoka kwa
Meneja wa Mradi wa Pori la Akiba la Selous Bw. Enock Msocha (wa tatu kushoto) mara baada ya
kuwasili kwa ajili ya kuwatembelea
Wafugaji 50 waliokolewa na Askari wanyamapori baada ya kutelekezwa na mtu mmoja waliyemtaja kwa jina maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa
kuwaonyesha njia ya mkato ndani ya Pori hilo na kisha kuwakimbia.
................................
Wizara ya Maliasili
na Utalii kupitia Askari wa Wanyamapori wa Pori la Akiba la Selous, Kanda ya Kaskazini
Mashariki Kingupira imewaokoa wafugaji
50 waliokuwa wakiwapitisha jumla ya ng’ombe 1780, kondoo 200 na punda 6
baada ya kutelekezwa kwa muda wa
siku tano na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la
Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya Pori hilo wao bila
kujua na kuamua kuwakimbia.
Bw. Lisasi Cherehani
ambaye ni mmoja wa wafugaji hao alisema ‘’tulimpa Mzigua kiasi cha zaidi ya
shilingi 5,000,000 kutoka kwa wafugaji kama malipo ya kutufikisha eneo la Ilonga
mkoani Morogoro tukitokea vijiji vya Ndundunyekanza, Kipungila na Chumbi vilivyopo wilayani Rufiji mkoani
Pwani kwa makubaliano kuwa atatupitisha njia fupi ya mkato tutakayotembea kwa muda wa
siku tano tu, hatukujua anatutupitisha ndani ya pori hili. ‘’
Baada ya kutelekezwa,
wafugaji hao ambao walikuwa katika hali
mbaya waliomba msaada kwa ndugu zao ambao waliwasiliana na Uongozi wa Pori la
Akiba la Selous ambao kwa haraka walifanya jitihada za kuokoa maisha yao ikiwa ni kuwapa huduma ya kwanza, maji, uji pamoja na kuwakimbiza hospitalini
kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi aliwatembelea wafugaji hao jana kwa
ajili ya kuwapa pole na kuwapelekea chakula yakiwemo maji pamoja na unga.
|
Post a Comment