Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo (kulia) akijadiliana jambo na Balozi Mpya wa Canada
nchini, Ian Myles wakati wa kikao
kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es
Salaam.
Na
Teresia Mhagama
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo amekutana na Balozi Mpya wa Canada nchini, Ian Myles kuzungumzia
masuala mbalimbali ya uendelezaji wa Sekta za Nishati na Madini nchini.
Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya
Nishati na Madini jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza kwa Balozi huyo
kufika wizarani tangu alipowasili nchini mwezi Agosti mwaka huu ili kuiwakilisha
nchi ya Canada.
Awali Balozi Myles alimweleza Profesa Muhongo kuwa
nchi hiyo imeshiriki katika shughuli mbalimbali za uendelezaji wa sekta za Nishati
na Madini nchini.
Mathalani, kupitia Shirika la Maendeleo la Canada (CIDA) nchi
hiyo ilikuwa ikitoa fedha kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini (TMAA) katika
mwaka wa Fedha wa 2012/2013 hadi
2015/2016 ili kuuwezesha Wakala huo kufanya shughuli zake za ukaguzi kwa
ufanisi pamoja na kujengewa uwezo kupitia mafunzo ambapo jumla ya fedha
zilizotolewa ni Dola za Canada 2500.
"Katika Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika
Mapato ya Madini, Gesi Asilia na Mafuta (TEITI), Canada ilishiriki katika kusaidia mchakato wa maandalizi ya kupata Sheria
ya kuongoza Tasnia ambayo ilipitishwa na
Bunge mwaka 2015. Pia tunawajengea uwezo
wataalam ili waweze kufanya kazi zao kwa
ufanisi," alisema Balozi Myles.
Aidha, alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi
zinazopewa kipaumbele na Serikali ya Canada katika masuala mbalimbali ikiwemo utoaji wa misaada ya
kifedha.
kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, alisema kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulianza tangu
miaka ya 1960 na kwamba nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika masuala
mbalimbali ikiwemo Kilimo na Elimu.
Alisema kuwa katika Sekta ya Madini, kampuni kubwa
zinazofanya shughuli za uchimbaji wa madini nchini, nyingi zinatoka nchini
Canada na kutoa mfano wa kampuni ya
uchimbaji madini ya Acacia na kwamba kodi zinazolipwa na kampuni hizo kwa Serikali,
zinasaidia kuendeleza miradi mingine ya
maendeleo.
Kuhusu uendelezaji wa Chuo cha Madini Dodoma
(MRI), Profesa Muhongo alimweza Balozi Myles kuwa mazungumzo kati ya Wizara na
Ubalozi huo kuhusu kukiendeleza Chuo hicho kuwa katika ngazi ya Polytechnic
yalikwishaanza hivyo alimweleza Balozi huyo kuwa ni vyema utekelezaji wa suala
hilo ukaanza.
" Tunataka
Chuo hiki kiwe cha kimataifa, kisiwe
kinatambulika hapa nchini tu na pia kiwe kinabadilishana wataalam na Vyuo
vingine vya nje ili kuboresha elimu inayotolewa katika Taasisi hiyo na pia
kijitegemee, badala ya kuwa chini ya mwavuli wa Wizara ya Nishati na Madini,”
alisema Profesa Muhongo.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaalika Wawekezaji
kutoka Canada kuja kuwekeza katika
utafiti na uchimbaji wa madini ya metali aina graphite na lithium kutokana
na umuhimu wake duniani na kutoa mfano kuwa madini ya graphite yanatumika kutengeneza vitu mbalimbali ikiwemo betri.
"Madini haya ya metali yana umuhimu sana kwa
sasa mfano ifikapo mwaka 1920-40 asilimia 40 ya magari duniani yatakuwa
yakitumia umeme hivyo ili kuwezesha hilo wanahitaji madini haya," alisema
Profesa Muhongo.
Pia alizialika kampuni za Canada kuja kuwekeza
katika uchimbaji wa madini adimu (rare
metals) ambayo yanahitajika katika teknolojia ya kisasa kama vile madini ya
titanium ambayo yanatumika katika kutengeneza
mitambo mbalimbali ikiwemo inayotumika kuzalishia umeme.
Pamoja na kualika makampuni ya Canada kuja
kuzalisha umeme nchini, Profesa Muhongo
alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi Myles ombi la Tanzania la kupeleka
wataalam wake nchini Canada kusomea masuala ya mafuta na gesi.
|
Post a Comment