Katibu wa chama hicho, Boniface Lameck, akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.
Na
Dotto Mwaibale
CHAMA cha Wahudumu wa Baa Tanzania (Chawabata) kimeiangukia serikali kwa
kuiomba iruhusu wenye mabaa kufanya biashara zao wakati wote ili kusaidia
kupata fedha za kulipa kodi na mishahara ya wafanyakazi wao.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Ali Huseein wakati
akizungumza Jijini Dar es Salaam leo asubuhi kuhusu changamoto waliyonao wenye
mabaa katika kufanya biashara yao hiyo ya uuzaji wa vileo na vinywaji baridi.
"Tunaiomba serikali kuangalia kwa karibu kuhusu muda wa kufungua baa kwani
muda huu wa sasa wa kufungua saa 10 jioni na kufunga saa tano ni mdogo
ukilinganisha na ilipokuwa awali wa kufungua wakati wote" alisema Hussein.
Hussein alisema nia ya serikali haikuwa mbaya ya kufungua baa saa 10 lakini
hawakuangalia upande wa pili wa wamiliki wa baa hizo kwani wengi wao kwani
katika muda huo wengi wao hawafanyi kabisa biashara.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara hao wanahitaji kupata muda wa siku nzima wa
kufanya biashara zao ili waweze kumudu kupata fedha za fedha za kulipa kodi ya
serikali na mishahara ya wafanyakazi na wahudumu wa baa ambao ni wengi ambapo
hivi sasa wanashindwa kufikia malengo.
Alisema baadhi ya baa zimepunguza wahudumu wake kutokana na kubanwa na muda huo
ambapo wahudumu wamekuwa wakiingia jioni tu baada ya muda wa asubuhi kupigwa
marufuku na serikali.
"Wenye mabaa hivi sasa wapo katika changamoto kubwa ya biashara zao
tunaiomba serikali kuangalia jambo hilo kwa sura nyingine ili kuinusuru
biashara hiyo kuanzia mmiliki wa baa na viwanda vinavyotengeneza bidhaa hiyo na
serikali yenyewe kupata kodi yake.
Alisema kuwa changamoto hiyo waliibaini baada ya kuzitembea baa kadhaa jijini Dar es Salaam mapema mwezi huu ambapo walipata fursa ya kuzungumza na wamiliki wa baa na wahudumu wa baa hizo.
Katibu wa chama hicho, Boniface Lameck alisema kutokana na kubanwa kwa muda wa
kufungua baa kumepunguza ajira kwa wahudumu wa baa nyingi hapa nchini ambao ni
wadau wao wakubwa wa viwanda vya bia na wamiliki wa baa.
Alisema bila ya wahudumu wa baa biashara hiyo inakuwa inapoteza kundi
muhimu la kuzifanya bia hizo kusambaa katika soko.
"Tunaiomba serikali kuruhusu baa kufunguliwa wakati wote kama ilivyokuwa
zamani jambo litakalosaidia wenye mabaa kupata fedha za kulipa mishahara na
kodi " alisema Lameck.
Lameck aliongeza kuwa muda uliotengwa na serikali ni kama masaa saba tu kuanzia
saa 10 hadi saa tano usiku na ndani ya muda huo wateja wengine wanaondoka
kuanzia saa moja hadi saa tatu hivyo kuwa changamoto ya biashara hiyo.
|
Post a Comment