Rais Mstaafu wa awamu ya nne
ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
Wakuu wa Vitivo wa Chuo hicho wakati wa kongamano la kusherehekea kutimiza
miaka 55 toka kuanzishwa kwa chuo hicho.
Na: Frank Shija,
MAELEZO
UONGOZI wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) takiwa kuhakikisha Chuo hicho kinaendelea kuwa
kiongozi miongoni mwa Vyuo Vikuu nchini.
Ushauri huo umetolewa
na Rais mstaafu wa awamu ya Nne ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akifungua maadhimisho
ya miaka 55 ya chuo hicho leo Jijini Dar es Salaam.
“Hiki ndicho Chuo
kiongozi kati ya Vyuo Vikuu vyote hapa nchini, mnatakiwa kuhakikisha
kinaendelea kuwa kiongozi huku Vyuo vingine vikifuatia”. Alisema Dkt. Kikwete.
Kwa upande wake
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Lwekaza Mukandara amesema
kuwa pamoja na changamoto zinazo kikabili chuo hicho wanaishukuru Serikali kwa
kuendelea kusaidia katika kuleta maendeleo ya chuo hicho.
Alisema kuwa baadhi
ya changamoto zimetatuliwa kwa pamoja kati ya Serikali na wahisani ambapo
alisema kuwa ujenzi wa kumbi mpya za mihadhara, Maabara za Kisasa na jengo la
malazi,pamoja na ujenzi wa hosteli za
wanafunzi unaoendelea katika Kampasi ya Julius K. Nyerere ambayo itakuwa na
uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 4000 mara itakapo kamilika.
Akiwasilisha mada juu
ya “hali ya Taaluma Barani Afrika katika Muktadha wa Kimataifa” Mhadhiri wa Heshima kutoka nchini Nigeria,
Profesa Tade Aina amesema kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni moja kati ya
Vyuo Vikuu mahiri barani Afrika ambapo kimetoa mchango mkubwa kwa ukombozi wa
nchi nyingi za bara hili.
Aliongeza kuwa yeye
binafsi ni mnufaika mkubwa wa UDSM kwani amekuwa na ushirikiano mkubwa na
baadhi ya wahadhiri kutoka chuo hicho katika masuala mbalimbali ya taaluma.
Jaji Mstaafu Joseph
Sinde Warioba ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wakati wa uwasilishaji mada alisema
kuwa kipindi Chuo hiki kinaanzishwa aina ya masomo yaliyokuwa yanafundishwa
chuoni hapo yalikuwa na muelekeo kuandaa wafanyakazi wa Serikali kwa wakati
huo.
Na kuongeza kuwa muelekeo
wa aina ya masomo uliendelea kubadilika kadri ya siku zilivyokwenda kutokana na
mabadiliko ya teknolojia na uhitaji wa soko la ajira.
Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kinaadhimisha miaka 55 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1961 kikiwa ni
tawi la Chuo Kikuu cha London, ambapo awali kilianzia katika mtaa wa Lumumba
kikiwa na wanafunzi 14 kabla ya kujengwa mahali kilipo sasa katika eneo la
Mlimani.
|
Post a Comment