Watendaji mbalimbali kutoka Serikali ya
Tanzania wakiwa katika kikao na Waziri
anayeshughulikia masuala ya Mafuta na Gesi wa DRC, Profesa Ngoyi Mukena
kilichofanyika jijini Tanga na kuhudhuriwa pia na Wataalam kutoka nchi hizo
mbili. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Dkt.
Mhandisi Juliana Pallangyo, wa kulia ni Kaimu Kamishna wa Nishati na Maendeleo
ya Petroli, James Andilile.
............
Serikali
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeeleza kuridhishwa kwake na uwezo
wa Bandari ya Tanga ambayo itatumika kupokea mafuta yatakayosafirishwa na Bomba
la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda.
Hayo
yamethibitishwa wakati wa kikao baina ya Waziri wa Nishati na Madini wa
Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri anayeshughulikia masuala ya Mafuta na Gesi wa DRC,
Profesa Ngoyi Mukena kilichofanyika jijini Tanga na kuhudhuriwa pia na Wataalam
kutoka nchi hizo mbili.
Waziri
huyo na ujumbe wake walifanya ziara katika Bandari hiyo baada ya DRC kuonesha
nia ya kusafirisha mafuta yake kwa Bomba hilo la Mafuta linalotoka Uganda hadi
Tanga baada ya kugundua Mafuta katika Ziwa Albert ambapo itakuwa ikisafirisha
mapipa 30,000 hadi Laki moja kwa siku.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema kuwa Ujumbe huo
utarudisha taarifa hiyo nzuri kwa Serikali ya nchi yao, aliongeza kuwa DRC wameahidi
kuwashauri wafanyabiashara wa DRC kuendelea kuitumia Bandari ya Tanga na Dar es
Salaam kwa shughuli za usafirishaji mafuta.
Pia,
Waziri Muhongo alisema kuwa, Ujumbe huo umepata fursa ya kutembelea eneo la
Chongoleani ambako inatarajiwa kujengwa gati itakayotumika kupakia mafuta ghafi
kwenye Meli baada ya kutoka Hoima nchini Uganda, ambapo pia walitembelea Bohari
za kuhifadhi mafuta ya kampuni ya GBP na kueleza kuwa, wafanyabiashara wa Kongo
wataendelea kutumia huduma za kampuni hiyo.
Mbali
na kuonesha nia ya utumiaji wa Bandari ya Tanga, Ujumbe wa DRC ulifika jijini Tanga
kwa lengo la kuomba Serikali hizo mbili kushirikiana katika utafiti na
uchimbaji wa mafuta na gesi Ziwa Tanganyika.
Katika
Kikao hicho Mawaziri hao walikubaliana kuwa, Wataalam wa pande mbili wanaosimamia Sekta
hiyo wakutane kwanza kwa lengo la kufahamishana taarifa mbalimbali za Ziwa
Tanganyika kuhusu rasilimali za gesi na
mafuta.
Vilevile,
Profesa Muhongo alieleza kuwa, baada ya Wataalam wa pande zote kukutana,
kitafuata kikao cha Mawaziri wa Sekta husika kwa ajili ya kuweka makubaliano ya namna ya kuendelea na
utekelezaji wa shughuli za utafiti na
uchimbaji wa mafuta Ziwa
Tanganyika.
Kwa
upande wake Waziri Mukena alikubaliana na mapendekezo ya Prof. Muhongo kuhusu Wataalam
wa DRC na Tanzania kukutana na kujadili
taarifa za Ziwa Tanganyika zitakazosaidia kutekeleza suala la utafiti wa
mafuta na gesi kwenye Ziwa hilo.
|
Post a Comment