Serikali yawataka Wadau wa Tasnia ya Habari Kutoa Maoni Kuhusu Muswada wa Habari
Na Beatrice Lyimo
SERIKALI imevitaka
wadau wa vyombo vya habari nchini kuacha kulalamika na badala yake waendelee
kutoa maoni yao kuhusu muswada wa sheria kwa vyombo vya habari ambao
unatarajiwa kuwasilishwaa katika Bunge lijalo mjini Dodoma.
Akizungumza katika
wakati tofauti wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi za Vyombo vya habari
nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO),
Hassan Abbas alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa muswada huo
unapitishwa na Bunge ili uweze kuwa sheria kamili na hatimaye kuifanya tansia
ya habari kuzidi kuheshimika.
Mkurugenzi Abbas
alisema tangu muswada huo uliposomwa kwa mara ya kwanza Bungeni, mwezi Septemba
mwaka huu, wadau wa tasnia ya habari
nchini ikiwemo Wahariri na waandishi wa habari wamekuwa mstari wa mbele
kupingana katika mitandao ya kijamii badala ya kutoa maoni yao katika mamlaka
zinazohusika.
“Ni aibu kwa maoni ya
muswada huu yanayohusu tasnia ya habari kutolewa na watu ambao hawana taaluma
ya habari, hivyo tukiwa kama wanataaluma ni vyema tujitokeze kwa wingi kutoa
maoni kifungu kwa kifungu ili kuweza kuboresha muswada” alisema Mkurugenzi Abbas.
Aliongeza kuwa
haitopendeza kwa muswada huo kuendelea kutolewa maoni na wananchi wengine na wadau
wa muswada kukacha kutoa maoni yao, na hivyo kusababisha muswada huo kuandikwa
na watu walio nje ya tasnia ya habari.
Abbas alisema, muswada
huo utakusudia kuiongezea nguvu tasnia ya habari kwa kuweka ikiwemo suala zima
la kuzingatia sheria na mipaka ya nchi katika utoaji wa habari na taarifa
maalum za Serikali kwa umma kwa kuzingatia ukomo wa kimataifa.
“Azimio la Umoja wa
Mataifa la mwaka 1948, pamoja na kuzungumzia kuhusu haki ya kupata taarifa
lakini pia limeanisha sheria mbalimbali ambazo hazina budi kuheshimiwa, na
sheria hizo ni pamoja na sheria za ulinzi na usalama” alifafanua Mkurugenzi
Abbas.
Akifafanua zaidi
alisema taaluma ya habari ni tasnia muhimu katika maendeleo ya taifa ila kwa
upande mwingine inaweza kuharibu maendeleo kwa njia moja au nyingine na hivyo
kuwataka wadau wa habari kujitokeza kutoa maoni kwa kujenga hoja za msingi ili
kuboresha muswada badala ya kulalamika.
Aidha kwa upande mwingine, Abbas alisema Ofisi yake ni mlezi
na mratibu wa vyombo vya habari na hawana budi kuwasiliana naye pindi
wanapopata changamoto mbalimbali ikiwemo utoaji na upatikanaji wa taarifa za
Serikali katika Wizara, Taasisi, Idara, Mikoa na halmashauri nchini.
Pia alisema zipo
taarifa ambazo zinahitaji kufanyiwa uhakiki ikiwemo ufundi na takwimu, na hivyo
aliwataka waandishi wa habari kuwa wavumilivu pale wanapohitaji taarifa hizo kutoka
kwa maafisa habari wa Wizara au Taasisi husika.
Kwa upande wake,
Mhariri Mtendaji wa gazeti la Majira, Imma Mbughuni alisema chombo hicho
kimejipanga kutoa maoni yao kuhusu muswada huo na mara baada ya kumaliza
wanatarajia kuwasilisha katika kamati ya kudumu ya Bunge.
Naye Mhariri Mtendaji
wa Gazeti la Jambo Leo, Anicetus Mwesa alisema chombo chao pia kimekusudia
kuupitia muswada huo ili kutoa maoni yao na baadae kuyawasilisha katika kamati
husika..
Post a Comment