( MAKALA ) Urafiki wa Rais Dkt JOHN MAGUFULI na Wajasiriamali Huu Hapa
Katika kampeni za takribani siku 60, Rais Magufuli aliahidi mambo mengi yakiwamo ya kusaidia na kuwainua watu wa kipato cha chini na hasa masikini ili kuhakikisha wanapata maendeleo.
Kauli hiyo amekuwa akiitoa kila mara alipokuwa akirudisha nidhamu serikalini, akitumbua majipu, akiwaajibisha watendaji wabovu na wala rushwa.
Katika kampeni yake ya kuwainua watu masikini, Rais Magufuli alitoa ahadi ya kuwainua wananchi hao wanaoishi vijijini kwa kuwapelekea mamilioni, yanayojulikana kama Mamilioni ya JPM.
Tunapotathmini mwaka moja wa kuwaongoza Watanzania na kukaa Ikulu ya Magogoni, Ilala, Dar es Salaam, Rais Magufuli, tunabaini kwamba amekuwa kipenzi na rafiki wa watu masikini na amekuwa mstari wa mbele kuwatetea wajasiriamali wadogo.
Ukweli huo umejidhihirisha kila mahali alipotembelea na kukutana nao, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha hawabughudhiwi na manispaa, wilaya na majijini kwa kutozwa kodi zisizoeleweka, kuhamishwa bila kuwaandalia miundombinu na mazingira rafiki ya kufanyia biashara.
Mfano mzuri Rais Magufuli ameutoa Julai 18, mwaka huu, wakati akiwaapisha polisi Ikulu Dar es Salaam, ambapo aliomba wamachinga wasisumbuliwe katikati ya jiji kwa lengo la kuwataka watafute riziki halali kwa kutumia biashara zao ndogo.
Rais Magufuli pia akiwa ziarani mkoani Mwanza, Agosti 12, 2016, aliwaagiza viongozi wa halmashauri na jiji hilo na Watanzania wote, kutowahamisha wamachinga, hadi pale halmashauri hizo zitakapokuwa zimeandaa miundombinu na mazingira rafiki ya kufanyia biashara na shughuli zao za uzalishaji.
"Hakuna kuondoa machinga mjini kwani huko nje mnakowapeleka hakuna wateja,” ilikuwa kauli ya Rais Magufuli iliyopokewa kwa shangwe na umati wa wakazi wa Mwanza uliofanyika katika Viwanja vya Furahisha.
Kauli hiyo ya Rais Magufuli, inaeleza wazi kuwa, amekuwa rafiki wa masikini, wafanyabiashara wadogo, mamalishe, babalishe na wajasiriamali wadogo, kwani amewataka wafanye shughuli zao za kupatia riziki bila kubughudhiwa, kusumbuliwa na kuhangaishwa na viongozi wa maeneo husika.
Rais Magufuli katika kuimarisha urafiki huo na wajasiriamali wadogo ambao wanatafuta riziki yao kwa kutoa jasho, bila mitaji na kuambulia kipato kidogo, ameamua kutegua kitendawili cha umasikini wao kwa kutoa Sh milioni 50 za maendeleo kwa kila kijiji nchini.
Kitendawili hicho hakika kitateguliwa na Rais Magufuli, kama ilivyo kawaida yake, ya kutekeleza ahadi nyingi na kwa muda mfupi, hivyo wajasiriamali kwa ujumla wao, wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo ambayo itatolewa vijijini kupitia vikundi mbalimbali vya ushirika.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa, amesema serikali itaanza kutoa fedha hizo kuanzia mwaka ujao wa fedha. Katika kuhakikisha ahadi hiyo inatekelezwa, Serikali tayari imetenga Sh bilioni 811, ambazo kabla ya kugawanya vijijini, imejikita katika kutafuta maoni ya wadau ili kuendesha mchakato huo tija na ufanisi.
Lengo ni kutorudia makosa yaliyofanyika katika ugawaji wa mabilioni, ambayo yaliishia katika mifuko ya wajanja. Ili fedha hizo ziwafikie walengwa katika miradi ya maendeleo yao, maoni ya wadau mbalimbali wa maendeleo yanatakiwa na wajasiriamali hao kwa kupewa mafunzo ya namna ya kuanzisha, kuendesha na kudumisha miradi hiyo ya maendeleo.
Walengwa kabla ya kupata fedha hizo, watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali ya namna ya kutumia fedha hizo ambazo ni muhimu katika kuanzisha, kuendeleza na kudumisha miradi ya maendeleo.
Serikali imewakutanisha viongozi wa halmashauri za wilaya, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), benki, mifuko ya hifadhi ya jamii na vikundi mbalimbali kutafuta namna ya kugawa fedha hizo. "Fedha hizo zitatolewa kwa awamu tatu katika kipindi cha miaka mitano,” alisema na kuongeza.
"Fedha hizo zitatolewa na kupelekwa benki kabla ya kutolewa kwa vikundi mbalimbali kama Vicoba na Saccos kulingana na taratibu zitakazowekwa."
Mchakato huo unaanza katika mikoa 10 nchini iliyo nyuma katika kutumia huduma za kifedha. Mikoa hiyo ni Singida, Lindi, Mtwara, Mbeya, Shinyanga, Geita, Kagera, Dodoma, Rukwa na Ruvuma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, amesema kabla ya fedha hizo kugawanywa katika vijiji, lazima kupata maoni ya wataalamu namna bora ya kutekeleza mpango huo.
Kaimu Mkurugenzi, Maendeleo ya Sekta Binafsi, Uwekezaji na Uwezeshaji, Ofisi ya Waziri Mkuu, Victor Mwainyekule, akizungumza kwa niaba ya Waziri Mhagama, amesema fedha hizo zinatolewa kwa lengo la kupambana na umasikini.
Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya Wanawake (TWB), Zablon Yebete, amesema mpango huo ni uwekezaji mkubwa kwa Watanzania unapaswa kuungwa mkono na vyombo vya fedha na wadau wengine nchini.
Kabla ya kutolewa fedha hizo, wamejitokeza matapeli, jambo ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekemea na kuwaonya wananchi kuwa makini na hao matapeli. Waziri Mkuu, Majaliwa, amewatahadharisha wananchi kuwa makini na kujiepusha na matapeli wanaopita katika maeneo yao na kuwataka wachange fedha za kuanzisha vikundi ili wapewe fedha hizo na serikali.
Majaliwa ametoa onyo hili katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Majimoto, Halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele mkoani Katavi, kwamba wananchi wanatakiwa kuwa macho na matapeli na mabilioni ya Magufuli.
“Serikali haijaanza kusambaza fedha milioni 50 za JPM. Jihadharini na hao matapeli na wezi hivyo wakija kwenye maeneo yenu wakamateni. Usambazaji huo ukianza mtajulishwa kupitia halmashauri zenu,” aliwasisitiza.
Onyo hilo la Waziri Mkuu, Majaliwa limekuja baada ya NEEC kutoa onyo kama hilo kuhusu baadhi ya taasisi na watu binafsi wanawadanganya wananchi kuwa fedha hizo zitapitia kwenye taasisi zao na kuwataka kujisajili nao ili waweze kufaidika na fedha hizo, jambo ambalo si la kweli.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i Issa amesema fedha hizo zimelenga kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (Saccos) na vikundi vya kifedha vya kijamii zikiwamo Benki za Maendeleo Vijijini (Vicoba) kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Mpango huo uliobatizwa jina la Fedha za Mfuko wa Mzunguko, unalenga kukabiliana na tatizo la mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mijini na vijijini.
“Watu na taasisi hizo zinazowadanganya wananchi zimekuwa zikiwatoza viwango mbalimbali vya fedha kwa kile wanachodai ni ada ya usajili ili vikundi hivyo vya wananchi viweze kusajiliwa na kutambuliwa kuweza kufaidika na mamilioni hayo kwa kila kijiji,” anasema Issa.
Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde amesema ahadi ya Rais ya Sh milioni 50 kwa kila kijiji itaanza kutekelezwa kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Serikali ya Awamu ya Tano imesisitiza kuwa itakuwa macho ili kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi iliyokusudiwa na kuwafikia walengwa, ambao watakuwa wamejiunga katika vikundi kama Saccos au Vicoba, wala si kila mtu mmoja mmoja.
Hivyo ili kupata mamilioni ya JPM ambaye ni rafiki wa watu masikini na wajasiriamali kwa ujumla, Watanzania wote wana wajibu wa kufanya, ni kujiunga katika vikundi na kuvisajili, ili vitambuliwe na vikubalike kisheria, Vinginevyo itakuwa vigumu kufikiwa na mamilioni hayo.
Post a Comment