Naibu Waziri Ofisi ya Rais , Tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo, akiwa na Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali akiambatana na viongozi wengine kukagua Zahanati ya Ziba. .............................
Kutokana na baadhi ya wananchi kuwafanyia vitendo vya ushirikina
watumishi katika Halmashauri mbalimbali nchini, Naibu Waziri Ofisi ya Rais ,
Tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo ameonyeshwa
kukerwa na tabia hiyo huku vimesababisha watumishi kupata msongo wa mawazo na
wengine kuomba kuhamishwa.
Jafo alitoa kauli hiyo alipokuwa akikagua zahanati mpya iliyopo
kijiji cha Ziba ndani ya Jimbo la Manonga wilayani Igunga mkoani Tabora na
alipokuwa akizungumza na watumishi wa wilaya hiyo.
Alimuagiza mkuu wa wilaya ya Igunga kutenga muda yeye na kamati
yake ya ulinzi na usalama kuwafikishia ujumbe wananchi wa wilaya ya Igunga
kuwakemea wenzao wenye tabia hiyo wilayani humo ili kuacha tabia hiyo ovu.
Jafo alisisitiza kwamba tabia hiyo imewasababishia baadhi ya
watumishi walio tendewa vitendo visivyo kupatwa na msongo wa mawazo na kuomba
kuhama maeneo walio pangiwa.
Naibu Waziri alisema kwamba jamii inapaswa kuwathamini watumishi
kwani wametoka maeneo mbalimbali ya nchi ili kuja kuwatumikia wao hivyo
wanatakiwa kuwathamini na kuwaheshimu kwa kulinda utu wao.
" Watani zangu mliopo hapa Wasukuma na Wanyamwezi mmepata
zahanati nzuri naomba muitunze. Pia sitaki kusikia daktari au mhudumu
amelala asubuhi anajikuta ng'ambo ya barabara au katika kiwanja cha
mpira,”alisema Jafo.
Kadhalika, alikemea kitendo cha sungusungu walio mchapa viboko
mwalimu mkoani humo huku akiwaagiza wakuu wa wilaya maeneo yote kupambana na
tabia za udhalilishaji wanazo fanyiwa watumishi wa umma katika jamii ili waweze
kufanya kazi kwa amani na kujiamini.
Aliwapongeza viongozi wa mkoa wa Tabora kwa umoja na ushirikiano
wao katika kuwaletea maendeleo wananchi wa mkoa huo.
|
Post a Comment