Mkazi wa Kilindi, Tanga Angela Basso, aliyetembea kwa miguu kwa muda wa siku 21 pamoja na Watoto wake Janeth Peter (9) na Happy Peter (7) kuja Mkoani Dodoma kuonana na Waziri mkuu ili kupeleka malalamiko yake ya kudhulumiwa mashamba yake ya hekari 30 na kuchomewa nyumba.
Na Augusta Njoji, Dodoma
Mkazi wa Kilindi mkoani Tanga, Angela Basso, akiwa na
watoto wake wawili Happy(7) na Janeth Peter(9), amelazimika kutembea kwa mikuu
kwa siku 21 hadi mkoani Dodoma kwa lengo la kumuona Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ili amsaidie kurudishiwa hekari 30 za mashamba yake aliyozoporwa.
Basso alifika mjini Dodoma akiwa na watoto wake hao, ambapo
alisema aliona ni vyema kwenda Dodoma kuonana na Waziri Mkuu kutokana na
kuporwa mashamba na kuchomewa nyumba yake katika kijiji cha Kwendigole wilayani
Kilindi na wanaume wawili ambao waliojitokeza kwa nyakati tofauti wakidai ni
maeneo yao.
Alisema alipita hatua zote zinazotakiwa kuomba mashamba, ambapo
awali alipatiwa hekari 10 na kijiji na akazifanyia shughuli za kilimo na
kujenga nyumba yake ya kuishi, lakini baada ya kwenda kujifungua alikuta mazao
yamefyekwa na yeye kutakiwa kuondoka kwenye eneo hilo.
Mwanamke huyo alisema baada ya kunyang’anywa alifikisha
malalamiko yake kuanzia uongozi wa kijiji hadi wilayani na baadaye akapatiwa
eneo jingine la hekari 20, lakini alijitokeza mtu mwingine na kudai eneo hilo
ni mali ya kanisa, licha ya kumiliki kihalali eneo la Hembekali.
“Nilikwenda kushtaki kwa serikali ya kijiji, kata na baadaye
kwenda kwa mkuu wa wilaya ambako iliamuliwa nirudishiwe mashamba yangu, lakini
hawakufanya hivyo mwisho wa siku nikafukuzwa kabisa kuishi kwenye eneo hilo,”
alisema Basso
Mwanamke huyo alisema baada ya kutimuliwa alianza kuishi maisha yake kituo cha
mabasi Muheza na baadaye alifukuzwa kituoni hapo kwa madai watu hawaruhusu
kulala ama kuishi hapo na ndipo akaamua kuanza safari ya Dodoma baada ya
kusikia Waziri Mkuu amehamia Dodoma.
Akisimulia machungu ya safari yake, Basso alisema akiwa njiani
walikuwa wakila mahindi ya kukaanga na maji ya kunywa na kulala porini muda
mwingine giza linapowakuta katikati ya pori.
“Naomba kusaidiwa jamani nimeanza kufuatilia tangu mwaka 2012 lakini bila
mafanikio jambo ambalo limechangia familia yake kusambaratika kutokana na
kukosa pa kuishi huku watoto wangu hawa wakikosa elimu kwa
kutangatanga,”alisema Mwanamke huyo.
Basso aliomba Serikali itende haki ili yeye aweze kupata haki
yake ya kurejeshewa mashamba yake na kurudi katika eneo hilo ili watoto wake
wawili wapate nafasi ya kusoma.
Mwanamke huyo alisema kwa sasa amekuwa kama mkimbizi kutokana na
kukosa hana mahali pa kuishi huku mumewe naye akiikimbia familia yake baada ya
kuporwa ardhi hiyo ambayo ilikuwa kama kitega uchumi chao.
|
Post a Comment