WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA, AKATAA KUGOMBEA TENA UBUNGE JIMBONI KWAKE
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amekataa ombi la wananchi wa jimbo lake la uchaguzi la Katavi la
kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili kuendeleza mipango
mbalimbali ya maendeleo aliyoianzisha.
Akizungumza baada ya Ibada ya
Jumapili katika kigango cha Kanisa Katoliki cha Kibaoni wilayani Mlele
(Jumapili, Julai 19, 2015), Waziri Mkuu Pinda amesema anamshukuru Mungu
kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka
minane na anaamini wakati umefika wa yeye kuwaachia wengine nafasi ya
ubunge wa jimbo la Katavi.
Amesema yeye ataendelea kuwa
karibu na wananchi wa Katavi wakati wote na kwa vile atakuwa na muda wa
kutosha atashiriki kikamilifu katika mikakati mbalimbali ya kuwaletea
maendeleo wananchi ili waweze kujikwamua kutoka kwenye umaskini.
Mheshimiwa Pinda aliwaasa
wananchi wa jimbo la Katavi wawe makini katika kuchagua mbunge na
madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu wasipewe nafasi katika
uchaguzi ujao.
Akimshukuru Mheshimiwa Waziri
Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani Mlele, Padri Aloyce Nchimbi
aliwaasa wananchi wa Wilaya ya Mlele kumuenzi Mheshimiwa Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda hata atakapokuwa amestaafu kwani bado watahitaji busara na
uzoefu wake katika kujiletea maendeleo.
Waziri Mkuu yuko kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele kwa ajili ya mapumziko mafupi.
Leo saa 10 jioni ndiyo mwisho wa kurejesha fomu za ubunge ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Post a Comment