RAIS KIKWETE AREJEA NYUMBANI, BAADA YA KUKAMILISHA ZIARA YA KIKAZI NCHINI USWISI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini
Dar es salaam mara baada ya kurejea nyumbani baada ya ziara ya kikazi
mjini Geneva.
PICHA NA IKULU
…………………………………………
Akiwa Geneva, Rais Kikwete
ameongoza vikao vya Jopo la Kimataifa Linalopendekeza Jinsi Dunia
inavyoweza kukabiliana na majanga yajayo ya magonjwa ya milipuko ambalo
kazi yake imeungwa mkono na nchi 21 ambazo zilichangia mapambano dhidi
ya ugonjwa wa Ebola.
Miongoni mwa mikutano ambayo Rais
Kikwete ameiongoza katika Makao ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini Geneva ni
pamoja na yeye na wanajopo wenzake kutoa maelezo kuhusu maendeleo ya
kazi yao kwa nchi ambazo zilichangia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola
katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Nchi hizo ambazo zimeunga mkono
kazi ya Jopo hili katika mkutano huo ni Venezuela, Umoja wa Ulaya (EU),
Uholanzi, Finland, Shirikisho la Russia (Russian Federation), Norway,
China, Ubelgiji, India, Ujerumani, Marekani, Uswisi, Canada, Brazil,
Denmark, Uingereza, Israel, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja
wa Afrika (AU), Benki ya Dunia (WB), Jamhuri ya Korea na Japan.
Pamoja na kwamba wajibu mkuu wa
Jopo hili siyo kuchunguza ugonjwa wa Ebola na madhara yake, bado ugonjwa
huo ni msingi mkuu wa kazi ya Jopo hilo ambalo wajibu wake ni kutumia
uzoefu wa Ebola kutoa mapendekezo ya jinsi dunia inavyoweza kukabiliana
na majanga ya magonjwa ya milipuko katika siku zijazo.
Ugonjwa wa Ebola ambao ulilipuka
katika nchi hizo tatu za Afrika Magharibi mwishoni mwa mwaka 2013 mpaka
sasa umeua watu 11,000 katika nchi hizo na kusababisha mshtuko mkubwa
duniani.
Hiyo ilikuwa mara ya 24 kwa
ugonjwa huo kulipuka katika Afrika tokea ulipolipuka kwa mara ya kwanza
mwaka 1976, miaka karibu 40 iliyopita, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC) wakati huo ikiitwa Zaire.
Hata hivyo, katika milipuko ya kwanza 23, ugonjwa huo uliua watu wachache zaidi kuliko mlipuko wa 24.
Jopo hilo limeambiwa kuwa tofauti
na matarajio ya dunia kuwa ugonjwa huo ulikuwa unamalizika katika nchi
hizo hasa katika Liberia, umeanza kupata kasi tena na nchi hizo tatu
zinakisiwa kuwa na wagonjwa karibu 70.
Jopo hilo lenye Wajumbe sita
liliteuliwa Aprili, mwaka huu, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Mheshimiwa Ban Ki Moon na kufanya vikao vyake vya mwanzo Mei, mwaka huu,
katika makao makuu ya UN, mjini New York, Marekani.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
akisalimiana na mfanyakazi wa Shirika la Ndege la Uswisi katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam mara baada
ya kurejea nyumbani baada ya ziara ya kikazi mjini Geneva.
………………………………………………………………………..
Mbali na kukutana na nchi
zilizochangia mapambano dhidi ya Ebola, Rais Kikwete na Jopo lake
limepata nafasi ya kumsikiliza aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya
Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, wakati ugonjwa huo unalipuka Dkt. Luis
Gomes Sambo wa Angola ambaye aliwaeleza wajumbe historia ya ofisi ya
kanda hiyo iliyoko mjini Brazzaville, Jamhuri ya Congo, katika
kukabiliana na ugonjwa huo.
Aidha, Wajumbe wa Jopo
wamemsikiliza Mkurugenzi mpya wa Kanda, Dkt. Matshidizo Rebecca Moeti
ambaye amezungumza kwa njia ya mkutanomtandao (teleconference) kutoka
mjini Brazzaville. Dkt. Moeti alianza kazi yake Januari Mosi, mwaka huu,
2015.
Vile vile, Wajumbe wa Jopo
wamesikiliza jitihada za Jamhuri ya Rwanda kukabiliana na magonjwa ya
mlipuko kupitia kwa Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Agnes Binagwaho ambaye
naye alizungumza kwa mkutanomtandao kutoka Kigali, Rwanda.
Nje ya vikao hivyo, Rais Kikwete
alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Mstaafu wa UN, Mheshimiwa
Kofi Annan. Katika mkutano huo kwenye Hoteli ya Intercontinental,
viongozi hao wawili wamezungumzia masuala mbali mbali ya kimataifa,
ikiwamo hali ya Burundi.
Rais pia amekutana kwa mazungumzo
na Mtendaji Mkuu wa Kituo cha South Centre ambacho kina makao yake mjini
Geneva, Dkt. Martin Kohr.
Kituo hicho kilianzishwa chini ya uongozi wa
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kwa nia ya utekelezaji wa Ripoti ya
Kamisheni ya Nchi Zinazoendelea (South-South Commission), ambayo iliongozwa na Mwalimu.
Post a Comment