Na Khamis Haji (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif
Hamad ametuma salamu za rambi rambi kwa wananchi wa India kufuatia kifo cha
mwanasayansi aliyewahi kuwa Rais wa nchi hiyo, Dk. Avul Pakir Abdul Kalam
kilichotokea Jumatatu iliyopita.
Ametuma salamu hizo wakati alipozungumza na Balozi mdogo wa
India hapa Zanzibar, Satendar Kumar huko katika ofisi za Ubalozi huo Migombani,
ambapo Maalim Seif alifika kusaini kitabu cha maombolezi.
Maalim Seif amesema Kiongozi huyo ni msomi aliyetoa mchango
mkubwa kwa Taifa la India hasa kutokana na mchango wake katika uvumbuzi wa
vyombo vya anga za juu, kwa ajili ya matumizi ya kiraia na Kijeshi.
Maalim Seif amesema bila shaka kifo chake kimeacha pengo na masikitiko
makubwa sio tu kwa wananchi wa India, bali kwa jamii ya wasomi Duniani, na amewataka
wananchi wa India kuwa na subira katika wakati huu mgumu wa maombolezi.
Abdulkalam (83) ambaye alipewa jina la umaarufu ‘mtu wa
misaili wa India’ alishika nafasi ya Urais wa India mwaka 2002 kwa muda wa
miaka mitano.
Post a Comment