CCM IMEKANUSHA UVUMI WA TAARIFA ZA MITANDAO YA KIJAMII
Siku za hivi karibuni kumeibuka
baadhi ya watu ambao wamekuwa kwa makusudi na kwa malengo maalum
wakitunga na kujiandikia taarifa, za uongo, kujenga hofu na au kupotosha
na kisha kuzisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kwa malengo
mahsusi dhidi ya Chama Cha Mapinduzi.
Watu hao katika nyakati tofauti
wamekuwa wakitengeneza uzushi na uongo huo na kuusambaza kwenye mitandao
pamoja na baadhi ya vyombo vya habari kwa lengo lisilo wazi.
Baadhi ya uzushi na uongo
uliotungwa na kusambazwa na watu au kikundi hicho ni pamoja na hii ya
leo inayoeleza mambo mbalimbali juu ya Ndugu Edward Lowasa na ambayo
watunzi wake wameandika kuwa imetolewa na Katibu wa NEC Itikadi na
Uenezi Ndugu Nape Moses Nnauye.
Ifahamike kuwa uzushi huo na
mwingine uliofanywa na watu au kikundi hicho umekusudia kujenga msukumo
ambao haupo ili kuujengea umma hofu ya huruma dhidi yao ili kusukuma na
kushinikiza agenda zao.
Jambo hilo ni uzushi mtupu kwa
sababu kwanza Ndugu Nape na wajumbe wote wa Sekretarieti hawapo jijini
Dar es Salaam badala yake wapo mikoani kushiriki katika zoezi la kura ya
maoni kwa ajili ya uteuzi wa wagombea Udiwani na Ubunge zoezi ambalo
litakamilika Agosti Mosi, 2015.
CCM inasisitiza kuwa habari hizo
si za kweli, zimeandikwa na watu kwa malengo binafsi ya kugombanisha,
kujenga chuki na uhasama baina ya Ndugu Nape, Chama, Wajumbe wa
Sekretarieti na wananchi kwa ujumla bila sababu.
Viongozi, wana-CCM na wananchi
kwa ujumla hawana budi kupuuza uzushi wowote ule unaotolewa na
kusambazwa na watu au vikundi vya hovyo vinavyotumiwa na watu kwa
maslahi binafsi, badala yake CCM itakuwa inatoa taarifa sahihi kwa
wakati ili kutoruhusu uwepo au kuibuka kwa ombwe la mawasiliano baina ya
umma na Chama.
Imetolewa na:-
Kitengo cha Mawasiliano na Umma
Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM
Lumumba, Dar es Salaam.
29/07/2015
Post a Comment