MWANAMUZIKI MACHACHARI “SHILOLE” AFUNGIWA MWAKA MMOJA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
kama msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini limemfungia msanii
wa Muziki wa Kizazi Kipya Zuena Mohamed kwa jina la kisanii Shilole
kufanya shughuli za sanaa nchini kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe
24/07/2015 hadi tarehe 24/07/2016.
...............................................................
Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe
09/05/2015 akiwa katika onyesho lake la Muziki nchini Ubelgiji alikiuka
maadili ya kazi ya sanaa mbele ya hadhira ya wapenda sanaa za Tanzania
na hivyo akadhalilisha utu wake na jamii ya Kitanzania kimaadili. Pia
itakumbukwa kwamba mnamo mwezi Oktoba, 2013 BASATA ilimuonya na akakiri
kwa kuomba msamaha kwa tabia yake ya kucheza bila kuzingatia utu na
maadili awapo jukwaani.
BASATA ilimpa nafasi ya kutoa
maelezo yake kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kitendo chake
cha kudhalilisha maadili, utu na sanaa ya Tanzania lakini akakaidi
kutoa maelezo. Hivyo basi BASATA imejiridhisha kwamba alikiuka maadili
ya kazi ya sanaa kwenye onesho lake la huko Ubelgiji makusudi na
amekiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa Sanaa.
Hivyo basi kutokana na ukiukwaji
huo wa sheria na kanuni za uendeshaji wa shughuli za sanaa nchini,
Baraza la Sanaa la Taifa chini ya Kanuni ya 30(1)(d) ya G.N 322 ya 2005
limemsimamisha kujishughulisha na kazi za Sanaa nchini kwa muda wa Mwaka
Mmoja tokea tarehe 24/07/2015.
Hivyo haruhusiwi kufanya au
kushiriki kwa namna yoyote ile shughuli yoyote ya onesho la sanaa nchini
au nje ya nchi. Iwapo atafanya kinyume cha hayo kutapelekea kupewa
adhabu zaidi ikiwa ni pamoja na yeyote yule utakaye shirikiana naye.
Ni matumaini ya Baraza la Sanaa
la Taifa kwamba wasanii na waandaaji wa shughuli za sanaa wataendelea
kutambua umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini.
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
Post a Comment