EDWARD LOWASSA KUGOMBEA URAIS KUPITIA CHADEMA
Baadhi ya washabiki wa waziri mkuu huyo wa zamani wakiwa wamefurika nje ya makao makuu ya Chadema kushuhudia tukio la uchukuaji wa fomu. |
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu wa zamani Edward
Lowassa, amechukua fomu kupeperusha bendera ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kimpitishe kugombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) ifikapo Oktoba 25 mwaka huu.
Katika Makao Makuu ya chama
chake hicho kipya leo Edward Lowassa alipokewa na maelfu ya watu
waliovalia sare za chama huku wakiimba wana imani naye.
Edward Lowassa aliwasili makao makuu mchana moja kwa moja akaenda ofisi za Katibu Mkuu Dk. Wilbroad Slaa.
Huku akisindikizwa na
Mwenyekiti Freeman Mbowe, Mwanasheria wa chama Tundu Lissu na Naibu
Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Edward Lowassa aliingia katika
ofisi hizo katika jukwaa maalumu la kupokea fomu.
Lissu ndiye alikuwa mzungumzaji
wa kwanza kwa kuwahakikishia wanachama hawakubahatisha kumpokea Lowassa
kwa sababu walifanya utafiti wa kina.
“Kamati Kuu imejiridhisha kwa
kushirikiana na viongozi wote wa juu akiwemo Katibu Mkuu na manaibu wake
wote wawili, Mwenyekiti na makamu wote wawili, wajumbe wa Kamati Kuu na
Mkutano Mkuu, kuwa Edward Lowassa ndiye kiongozi tunayemtaka hivyo
Jumapili iliyopita tuliitisha Kamati Kuu ya dharura kumpitisha,” alisema
Lissu.
Baada ya kukabidhiwa fomu
aliyolipiwa na wanachama waliochangishana fedha hadi kufikia Sh milioni
moja, Edward Lowassa alisimama kuwasalimia waliohudhuria kwa kuwaahidi
kufanya kazi kwa juhudi ili kuiondoa Tanzania katika hali mbaya ya
kiuchumi.
“Nashukuru kwa kunipa heshima
kubwa namna hii, sina maneno ya kuwashukuru zaidi ya kuahidi kufanya
kazi kwa bidii ili iwe malipo ya mlichonifanyia.
“Shukurani yangu itakuja baada
ya kushinda uchaguzi, lakini ushindi hauji bila umoja. Chadema inaweza
kuleta mabadiliko kupitia ukawa.
Baada ya kumaliza kuzungumza
alisimama Mbowe kutoa neno la shukurani kwa Edward Lowassa kwa kusema
Chadema kitaendelea kuwa chama makini kinachosimamia maamuzi yake.
Vilevile alizungumzia ratiba ya
vikao vya kujadili fomu ya mgombea ambaye mpaka sasa ni Edward Lowassa
pekee, “Vikao vitaanza Agosti mbili kujadili namna tutakavyoingia katika
uchaguzi mkuu.
“Baraza Kuu litaketi Agosti
tatu kujadili fomu ya mgombea na kujadili ilani ya uchaguzi, Mkutano
Mkuu utafanyika Agosti nne kupitisha jina la mgombea na mgombea mwenza.
“Vikao vya kamati Kuu
vitaendelea tarehe tano, sita hadi saba kuidhinisha wagombea wa ubunge
kwa kushirikiana na Ukawa. Kazi ya kujadili wagombea si ndogo nawaomba
waandishi wa habari muwe wavumilivu msipige ramli,” alisema Mbowe.
Baada ya kumalizika hafla hiyo Edward Lowassa alitoka nje kwa ajili ya picha ya pamoja kuwaonyesha wanachama fomu yake.
Post a Comment