Header Ads

Shirika la Ndege la ATCL latakiwa Kubadilisha Menejiment yake ili Kuongeza Ufanisi

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Menejimenti na Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Eng. Ladislaus Matindi akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), wakati Waziri huyo alipokutana na menejimenti ya shirika hilo pamoja na wafanyakazi wake jijini Dar es Salaam.

Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), alipozungumza na uongozi wa Shirika hilo na Wafanyakazi jijini Dar es Salaam.
.........................................

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kufanya mabadiliko katika menejimenti ya Shirika hilo ili kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji kazi.

Ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa Shirika hilo na kuwataka kutoa huduma bora ili kulifanya Shirika hilo kuwa miongoni mwa mashirika bora  ya ndege barani Afrika.

“Nataka ndani ya mwezi mmoja uwe umeshafanya mabadiliko katika menejimenti, mabadiliko lazima yaanzie juu kwanza kwa watoa maamuzi na ishuke hadi kwa wafanyakazi wazembe na wasio waadilifu”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amepinga nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa Shirika hilo hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika juhudi za kulifufua na kuliimarisha Shirika hilo.

Aidha Waziri Mbarawa ameitaka Idara ya Masoko ya shirika hilo kuzunguka katika taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake na kuzishawishi kuweza kutumia huduma za usafiri wa anga wa ATCL.

“Serikali imekamilisha upande wake wa ununuzi wa ndege, sasa kazi inabaki kwenu, sitaki watu wa masoko kukaa ofisini”, amesema Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa wafanyakazi wa ATC wanatakiwa kujipanga kutoa huduma iliyotukuka kwa wateja wake ili kuweza kuhimili ushindani uliopo katika mashirika ya ndege nchini.

“Inabidi tofauti kubwa ionekane kati yenu na mashirika mengine, yeyote ambaye anaona hawezi kutoa huduma bora kwa mteja atafute sehemu nyingine kwani hapa hatufai ”, amesisitiza Waziri Mbarawa.

Profesa Mbarawa amelitaka shirika hilo kutumia mfumo wa kisasa wa kukata tiketi kwa njia ya simu na kompyuta ili kuwarahishia watumiaji wa shirika hilo kuweza kupata tiketi kwa haraka na urahisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Eng. Ladislaus Matindi amemhakikishia Waziri Mbarawa kufanyia kazi maagizo aliyotoa na kuahidi kuboresha utendaji kazi  wa shirika hilo kwa lengo la kuteka soko la ushindani wa usafiri wa anga nchini.


“Kwa sasa tumeanza vizuri na naamini uwezo wa kuzalisha faida zaidi tunao, tunaahidi kuboresha utendaji kazi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Tano”, amesema Eng. Matindi.

No comments

Powered by Blogger.