Header Ads

Wanafunzi wa Shule za Sekondari Watakiwa Kuwa Mabalozi wa Elimu ya Mpiga Kura

 Afisa Uchaguzi wa NEC Bw. Stephen Elisante akiwaonyesha wanafunzi wa shule ya Sekondari Kidinda fomu maalumu zinazotumika kujaza matokeo ya uchaguzi katika vituo vya kupigia kura wakati akitoa elimu ya Mpiga Kurra kwa wanafunzi wa shule hiyo, Bariadi mkoani Simiyu.

 Mwanasheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),Bi. Fausta Mahenge akitoa elimu ya mpiga kura kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria yanayosimamia chaguzi za Tanzania kwa wanafunzi 743 wa  Shule ya Sekondari Kidinda wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

 Afisa Uchaguzi wa NEC Bw. Stephen Elisante akisisitiza jambo kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Kidinda wakati akitoa elimu ya Mpiga Kurra kwa wanafunzi wa shule hiyo, Bariadi mkoani Simiyu.

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kidinda Mwalimu Paul Susu akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo mara baada ya kuwakaribisha Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi waliofika shuleni hapo kutoa Elimu ya Mpiga Kura kwa wanafunzi wapatao 743 wa shule hiyo.

 Mwanasheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),Bi. Fausta Mahenge akiwaonesha mfano wa karatasi inayotumika kupigia kura yenye majina ya wagombea wa vyama mbalimbali wakati akitoa elimu ya Mpiga Kura katika Shule ya Sekondari Kidinda wilayani Bariadi mkoani Simiyu.

 Mwanafunzi wa Kidato cha tatu wa shule ya Sekondari Kidinda, Filipo Madeni akiwauliza swali Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu mfumo unaotumika kuwapata wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Kidinda wakifuatilia kwa makini darasa la Elimu ya Mpiga kura kutoka kwa maofisa wa NEC walioitembelea shule hiyo. 


Na Aron Msigwa – Bariadi-SIMIYU.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa wito kwa wanafunzi wa shule za Sekondari waliopatiwa elimu ya Mpiga Kura katika maeneo mbalimbali nchini kuwa mabalozi wazuri wa kuifikisha elimu waliyoipata  kwa  jamii inayowazunguka.

Wito huo umetolewa na Mwanasheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bi. Fausta Mahenge wakati akitoa elimu ya mpiga Kura na kuhusu masuala ya kisheria na utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Kidinda Bariadi mkoani Simiyu.

Amewaeleza wanafunzi hao  kuwa NEC imezindua programu ya kuwafikia wanafunzi wa Shule za Sekondari na vyuo Vikuu ambayo haikuwepo hapo awali ili kuwafikia vijana wengi zaidi kwa kuzingatia nafasi ya vijana katika kufikisha elimu hiyo katika ngazi ya familia, mitaa na vijiji.

“ Baada ya elimu hii nawaomba muwe mabalozi wa elimu ya mpiga kura katika maeneo yenu, ninajua ninyi mmetoka katika mitaa na vijiji mbalimbali, mkawe mabalozi wa kuelezea kazi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika ngazi za familia zenu ili tusaidiane kufikisha ujumbe na kuiwezesha Tanzania kusonga mbele” Amesisitiza Bi. Fausta.

Amesema tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka 2015,  NEC imekuwa ikitekeleza programu endelevu za kutoa elimu ya mpiga kura katika maeneo mbalimbali ili kuongeza uelewa kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kufanikisha chaguzi mbalimbali zinazofanyika  na  Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2020.

Ili kufanikisha lengo hilo Tume itashirikiana na Asasi mbalimbali za Kiraia ambazo zitapewa vibali maalumu ili kutoa elimu ya mpiga kura  katika maeneo mbalimbali nchini.  

Akitoa ufafanuzi wa kuhusu maswali yaliyokuwa yakiulizwa na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mipaka yake na maamuzi ya kisheria yanayochukuliwa na baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi amesema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweka wazi mamlaka ya Tume katika kusimamia na kuratibu shughuli za chaguzi nchini za kidemokrasia hapa nchini.

 Amesema kwa mujibu wa sheria NEC inaratibu na kusimamia Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na kutangaza matokeo ya ngazi hizo kwa upande wa Tanzania Bara na kufafanua kuwa chaguzi za viongozi wa Serikali za mitaa zimeachwa chini ya  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

“Kwa upande wa Serikali za Mitaa, Sheria haiipi mamlaka Tume ya kusimamia chaguzi hizo badala yake uchaguzi wa Serikali za Mitaa uko chini ya Wizara inayohusika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeachiwa jukumu hilo” Amesema.

Kuhusu kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi amefafanua kuwa Mahakama inaweza kubatilisha matokeo ya mgombea yoyote pale taratibu za uchaguzi zinapokiukwa pia mgombea aliyepitishwa kwa nafasi husika kugundulika kuwa amekosa sifa hali inayosababisha matokeo yake  kubatilishwa na Mahakama.

Kwa upande wake Afisa Uchaguzi wa NEC Bw. Stephen Elisante akielezea historia ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) amesema kuwa ilianzishwa mara baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1993 na kuongeza kuwa kuwa Ibara ya 74 kifungu cha 6 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza majukumu ya NEC ikiwemo kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapigakura na kusimamia uendeshaji wa uchaguzi Tanzania Bara.

Amewaeleza wanafunzi hao kuwa NEC ina mamlaka ya kuchunguza mipaka na kuigawa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vikiwemo vya idadi ya watu, hali ya kiuchumi ya eneo na ukubwa wa eneo husika.

Naye Afisa Habari wa NEC Bi. Margareth Chambiri akitoa ufafanuzi kuhusu programu ya NEC ya kutoa elimu ya mpiga kura amesema kuwa NEC itaendelea kuwafikishia elimu ya Mpiga kura wananchi ili kuongeza uelewa wa wananchi na kuondoa baadhi ya dosari zilizojitokeza kwenye chaguzi zilizopita kabla ya uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2020.

“Licha ya changamoto mbalimbali za Kijiografia katika kuwafikia wananchi tungependa kuona idadi kubwa ya vijana na wananchi wanajiandikisha  na kujitokeza kupiga kura, naomba vijana mshiriki kikamilifu katika kuwaelimisha wananchi kwa kuwa hii ndio Demokrasia tunayoitaka Tanzania vijana mliopata elimu leo muwe chachu kwa wenzenu ili tuongeze idadi ya wapiga kura na wagombea katika miaka ijayo” Amesisitiza.

Kwa upande wao walimu na wanafunzi wa shule hiyo wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kumalizika kwa program ya utoaji wa elimu ya mpiga kura katika shule hiyo wameishukuru NEC kwa kuwapatia elimu  wanafunzi hao.

Wamesema hatua ya NEC kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule hiyo inaongeza uelewa kwa wanafunzi wa shule hiyo katika somo la Siasa na kuwafanya wanafunzi hao kuwa raia na wapiga kura wema.

Wameiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendelea kutoa elimu hiyo kwa vijana wengi zaidi ili kuwawezesha kuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu sahihi ya Mpiga Kura katika maeneo mbalimbali nchini.


No comments

Powered by Blogger.