Abiria wakiteremka katika Kivuko cha Mv Kome II kinachotoa huduma kati ya Nyakarilo na Kome wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
.................
Na Theresia Mwami TEMESA Mwanza
Mtendaji Mkuu TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu amemuagiza Meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Ferdinand Mishamo kuwafuta kazi mara moja watumishi sita wa kivuko cha Mv Kome kuanzia 11/10/2016 pamoja na kuwapa onyo kali watumishi wengine wawili wa kivuko hicho kwa kuondoka katika eneo la kazi bila ruhusa ya mkuu wao wa kazi.
Ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha TEMESA mkoani Mwanza na kutembelea kivuko cha Mv Kome kinachotoa huduma ya usafiri kati ya Kome na Nyakarilo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
Dkt Mussa Mgwatu pia amemwagiza Meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Ferdinand Mishamo kuhakikisha wafanyakazi wa karakana na kivuko wanawajibika ipasavyo ili kuondoka na uzembe kama uliojitokeza.
“Hatuwezi kuvumilia uzembe namna hii watumishi wanaamua tu kuondoka eneo la kazi bila kupata ruhusa kutoka kwa wakuu wao hii sio sawa kabisa na nakuagiza Meneja hawa watumishi waache kazi mara moja” alisisitiza Dkt Mgwatu.
Aidha Dkt Mussa Mgwatu amemwagiza Meneja wa TEMESA Mwanza kuajiri watumishi wengine ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi kwa kuzingatia weledi na uwajibikaji wawatumishi watakao waajiri.
Kwa upande Meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Ferdinand Mishamo alikiri kuwa hakukuwa na ruhusa yoyote ya maandishi iliyotolewa kwa watumishi kutokuwepo kazini siku hiyo.
“Mtendaji sina barua yoyote kutoka kwa watumishi hawa iliyofika kwangu kuomba ruhusa ya kutokuwepo katika kituo cha kazi.” alisisitiza Mhandisi Mishamo.
Mhandisi Ferdinand Mishamo amewaja watumishi waliachishwa kazi kuwa ni walinzi wanne Bw. Apolinary Kapulula, Bw. Marwa Nchagwa , Bw. Msomi Stanley na Joseph Mtokambali, wengine ni Bw. Baharia Geofrey Biseko na Mkusanya Mapato wa kivuko hicho Bw. Elisha Mbondo.
Amewataja Watumishi wanaopewa onyo kali ni Mkuu wa Kivuko cha Mv Kome Bw.Elias Mabushi na dereva wa kivuko hicho Bw.Juma Bugingo.
Dr. Musa Mgwatu yupo katika ziara ya kutembelea vituo vya TEMESA vilivyopo Kanda ya Ziwa ili kubaini changamoto zilizomo na kuzitafutia ufumbuzi.
|
Post a Comment