Header Ads

Wanawake 47 wahitimu mafunzo ya ukataji na ung’arishaji Vito Jijini Arusha

Mkufunzi Msaidizi katika Kituo cha Jemolojia Arusha, (TGC), Lilian Petro (wa kwanza kulia) akionyesha madini ya vito yaliyong’arishwa na wanafunzi wanaopata mafunzo katika Kituo hicho kilicho chini ya Wizara ya Nishati na Madini. Wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthamini wa Madini ya Almasi na Vito (TANSORT), Archard Kalugendo, wa Pili kushoto ni Mhe. Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) na wa kwanza kushoto ni Beatrice Lupi, Mhasibu Mkuu kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
.............................

Imeelezwa kuwa jumla ya wanawake 47  wamehitimu mafunzo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito yanayotolewa na Kituo cha Jemolojia jijini Arusha ambacho kipo chini ya Wizara ya Nishati na Madini.

Hayo yalisemwa jijini Arusha na Kaimu Mratibu wa Kituo hicho, Erick Mpesa wakati wa Mnada wa Pili wa Kimataifa wa Madini ya Tanzanite unaofanyika jijini Arusha katika Kituo hicho.

Mpesa alisema kuwa mafunzo hayo yalianza kutolewa mwaka 2014 ambapo katika Awamu ya kwanza wanafunzi 15 walihitimu, Awamu ya Pili walihitimu  wanafunzi 14 na Awamu ya Tatu walihitimu wanafunzi 18.

“Mafunzo haya hutolewa kwa muda wa miezi Saba  ambapo Wanafunzi hawa ambao huwa na  umri wa chini ya miaka 30 wanafadhiliwa na Mfuko wa Kuwaendeleza Wanawake chini ya Kamati ya Maonesho ya Vito ya Arusha (AGF) na Wizara ya Nishati na Madini,” alisema Mpesa.

Mratibu wa TGC aliongeza kuwa Kituo hicho  pia kinaendesha shughuli  za uchongaji wa mawe ya miamba kwa kutengeneza vinyago vyenye maumbo mbalimbali kama ya wanyama, ndege, samaki na vitu mbalimbali vya urembo.

Mmoja wa wanafunzi katika Kituo cha Jemolojia Arusha, Zuwena Mtoo, akionesha utaalam wa kukata na kung’arisha madini ya Vito, baada ya kupata mafunzo katika Kituo hicho kilicho chini ya Wizara ya Nishati na Madini. 

Samadu Mohamed, kutoka Kituo cha Jemolojia Arusha, akionesha moja ya vinyago vinavyotokana na mawe ya miamba vinavyotengenezwa katika kituo hicho.

No comments

Powered by Blogger.