Wakimbizi kutoka nchini Burundi walioko katika kambi ya Nyarugusu wakiwa
wamebeba shehena ya unga wa mahindi jana, muda mfupi baada ya kugawiwa chakula
hicho Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia chakula (WFP), lililoweka
kituo chake katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu, mkoani
Kigoma.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
IDADI YA WAKIMBIZI WA BURUNDI WANAOHIFADHIWA KATIKA KAMBI YA WAKIMBIZI
YA NYARUGUSU YAONGEZEKA
Idadi ya wakimbizi kutoka Burundi wanaokimbia nchi yao na kuingia
nchini Tanzania imefikia 91,661 kwa takwimu za Jumanne, tarehe 08 Septemba,
2015. Wakimbizi hawa kwa sasa
wamehifadhiwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu
mkoani Kigoma.
Tangu waanze kuingia mwezi Aprili mwaka huu, Wizara ya Mambo
ya Ndani ya nchi kwa kushirikiana na
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine
imekuwa ikiwapokea na kuwapa hifadhi na huduma nyingine muhimu. Huduma hizi ni pamoja na za ulinzi, chakula,
maji, elimu na afya.
Kutokana na kuboreshwa kwa huduma za ulinzi, hali ya ulinzi
na usalama katika kambi ya Nyarugusu na maeneo yanayoizunguka imeimarika ambapo
upo usalama wa kutosha. Kazi hii inafanywa na Polisi kwa kushirikiana na
vikundi vya ulinzi shirikishi vinavyojumuisha baadhi ya wakimbizi wanaoishi
katika kambi hii.
Kuhusu huduma za afya, Serikali kwa kushirikiana na wadau
wengine kama vile Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) imeimarisha
huduma hizo kwa kuongeza idadi ya watendaji, vifaa na dawa. Kuimarishwa kwa
huduma za afya kumesaidia kudhibiti magonjwa ya mlipuko na kukabiliana na
magonjwa mengine yasiyo ya mlipuko.
Upatikanaji wa maji safi na salama na kutolewa kwa elimu ya usafi wa
mazingira pia umesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Wakati huohuo huduma za elimu zimeimarishwa ambapo kiasi cha
wanafunzi 3,889 wa elimu ya msingi na sekondari waliokuja na wazazi wao kutoka
Burundi wameandikishwa na wanaendelea na masomo.
Kabla ya kufikia idadi hii ya sasa, wengi wa wakimbizi hawa
walianza kuingia kwa maelfu kupitia kijiji c,,ha Kagunga kilichopo mpakani na
nchi ya Burundi ambapo idadi ilianza kupungua kidogo kidogo lakini kwa siku za
hizi karibuni wakimbizi hawa wameendelea kuingilia wakiwa katika vikundi
vidogovidogo kupitia katika vijiji vingine vya mpakani na nchi ya Burundi.
Vijiji hivyo ni pamoja na Kilelema, Kitanga, Helushingo,
Migongo,na Kigadie vilivyopo wilayani Kasulu na Mabamba na Katanga wilayani
Kibondo na Kituo kidogo cha Uhamiaji cha Manyovu kilichopo mpakani na nchi ya
Burundi. Aidha wakimbizi wengine
wamekuwa wakipitia vijiji vya Bugarama, Kabanga na Kasange vilivyopo wilayani
Ngara mkoani Kagera.
|
Post a Comment