Header Ads

Sekondari Nchini Zashauriwa Kuwekeza katika Matumizi ya BIOGAS

Mtaalam wa Nishati Endelevu na mabadiko ya Tabia nchi Bw. Shima Sango kutoka Taasisi ya Uendelezaji wa Nishati asilia na Uhifadhi wa Mazingira (TaTEDO) Akiwasha moja ya jiko la gesi liliojengwa katika shule ya Sekondari Manzese.
Mtaalam wa Nishati Endelevu na mabadiko ya Tabia nchi Bw. Shima Sango kutoka Taasisi ya Uendelezaji wa Nishati asilia na Uhifadhi wa Mazingira (TaTEDO) Akiwasha moja ya jiko la gesi liliojengwa katika shule ya Sekondari Manzese.
Meneja Uhusiano wa Jamii wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) Bi.Neli Msuya akielezea ushiriki wa DAWASA katika kufanikisha ujenzi wa Mradi wa Biogesi katika shule ya Sekondari Manzese ya jijini Dar es salaam mara baada ya kutembelea mradi huo jana jijini Dar es salaam.
talaam wa masuala ya Biogesi na Majiko Sanifu wa Taasisi ya kuendeleza Nishati Asilia na Uhifadhi wa Mazingira Tanzania ( TaTEDO) Bw.Stephen Boniface akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu ujenzi wa mtambo wenye uwezo wa kuzalisha gesi yenye mita za ujazo 200 walioujenga katika shule  ya Sekondari Manzese iliyoko wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam jana. Kulia kwake ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Manzese Bw.Linus Mwakasege.

Na.Aron Msigwa-MAELEZO

Shule za Sekondari kote nchini zimeshauriwa kuwekeza katika matumizi ya Nishati endelevu ya Biogesi na majiko sanifu ili kulinda na kuhifadhi mazingira.

Ushauri huo umetolewa na Meneja Uhusiano wa Jamii wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam  (DAWASA) Bi.Neli Msuya mara baada ya kutembelea ujenzi wa Mradi wa kuzalisha Nishati endelevu ya Biogesi katika Shule ya Sekondari Manzese wilayani Kinondoni, jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam ( DAWASA ) ikishirikiana na Taasisi ya Kuendeleza Nishati Asilia na Uhifadhi wa Mazingira (TaTEDO)na  Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa UN- HABITAT wameamua kuitumia changamoto  ya uhifadhi wa Maji Taka iliyokuwa inaikabiri shule hiyo kwa kuanzisha mradi wa kuyageuza maji taka ya vyoo vya shule hiyo kuwa rasilimali ya kuzalisha nishati endelevu ya Biogesi.


Bi.Neli ameeleza kuwa TaTEDO inajenga miundombinu ya mradi huo chini ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) na kuongeza kuwa  mradi huo unatarajiwa kuanza kufanya kazi mwezi Desemba mwaka huu.

Amesema matumizi ya gesi hiyo yataimarisha utoaji wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosoma michepuo ya Sayansi kupitia maabara ya kisasa inayojengwa shuleni hapo.

"DAWASA tunauona mradi huu kama mkombozi kwa wanafunzi hawa na  mfano wa kuigwa kwa shule nyingine zilizoko ndani na nje ya jijini Dar es salaam zinazokabiliwa na uhaba wa nishati ya umeme  na gesi, natoa wito kwa shule nyingine kuanza kutumia nishati endelevu ya Biogesi ili klinda na kuuhifadhi mazingira" Amesisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Manzese Bw. Linus Mwakasege akitaja faida za mradi huo amesema utawasaidia kupunguza gharama za matumizi ya mkaa, kutunza mazingira na kuondoa harufu mbaya ya vyoo iliyokuwa ikiwasumbua wanafunzi wa shule hiyo.

Amesema shule yake ina idadi ya wanafunzi 1400 hivyo matumizi ya  gesi hiyo yatawasaidia wanafunzi wanaojifunza masomo ya sayansi katika maabara iliyoko shuleni hapo ambayo imewekewa mifumo ya kusambaza gesi hiyo na kuongeza kuwa  baadhi ya shule zimeanza kwenda kujifunza  kuhusu mradi huo.

Naye Mtalaam wa masuala ya Biogesi na Majiko Sanifu wa Taasisi ya kuendeleza Nishati Asiliana Uhifadhi wa Mazingira ( TaTEDO) Bw.Stephen Boniface wasimamizi wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha gesi katika shule hiyo amesema kuwa kiwango cha gesi asilia inayozalishwa kimefikia mita za ujazo 200.

Amesema kuwa wao kama Taatedo kazi waliyoifanya ni kuunganisha mabomba katika vituo viwili vya kukusanyia taka kwa ajili ya kuanza kuzalisha gesi itakayotumika kupikia, maabara na mambo mengine.

Amesema TaTEDO wamefanya kazi bega kwa bega na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) ili kuwezesha kiasi kikubwa cha maji taka yanayotoka katika vyoo vya shule hiyo kuzalisha gesi na wakati mwingine kutibiwa ili yaweze kutumika kwa shughuli za umwagiliaji wa bustani.

No comments

Powered by Blogger.