Header Ads

Profesa MBARAWA aunda Tume ya Wataalamu Ujenzi wa Terminal III

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari, (hawapo pichani), mara baada ya kukagua ujenzi wa Jengo la tatu la Abiria (TB III), jijini Dar es Salaam.
............................

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameteua timu mpya ya wataalamu saba kwa ajili ya kusimamia mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III), katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Hatua hiyo imefikiwa kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais John Magufuli alilolitoa jana wakati alipofanya ziara ya kushtukiza uwanjani hapo  kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika mradi huo.

Timu hiyo inaongozwa na Eng. Julius Ndyamukama inaundwa na  Eng, Godson Ngomuo, Eng. Humphrey Kanyenye, Eng. Abednego Lyanga, Eng. Mbila Mdemu na Eng. Rehema Myeya.

“Naamini timu hii ina wataalamu mahiri, hivyo itasimamia ujenzi huu kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha (value for money”, amesema Waziri Mbarawa.

Profesa Mbarawa amemhakikishia mkandarasi wa kampuni ya BAM kutoka uholanzi inayojenga jengo hilo kuwa Serikali itamlipa mkandarasi huyo katika kipindi cha wiki mbili kutoka sasa.

Aidha, ameitaka timu hiyo kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo unakamilika mwezi Desemba mwaka huu kama ilivyopangwa.

Mafundi wa Kampuni ya BAM wanaojenga jengo la tatu la Abiria (TB III) wakiendelea na kazi ya ujenzi, jijini Dar es Salaam. Kazi ya ujenzi zimeanza baada ya kutarajiwa kusimama sababu ya kukosekana fedha ambapo Serikali imesema itatoa fedha za kukamilisha mradi huo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kushoto), akitoa maelekezo kwa timu aliyoiteua kusimamia ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria (TB III), mara baada ya kuteuliwa leo jijini Dar es Salaam. 

No comments

Powered by Blogger.