Header Ads

Wafanyabiashara wa Asali Wilayani Ikungi wapewa Mwezi Mmoja Kuhamia Jengo Jipya

                             
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akizungumza na wadau wa asali wakiwemo wazalishaji na wafanyabiashara  katika uzinduzi wa vifungashio vya asali wilayani humo.
   ..........................................

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu ametoa mwezi mmoja kuanzia leo  kwa wafanyabiashara wote wanaouza asali pembezoni mwa barabara kuu ya Singida-Dodoma kuhamia katika jengo lililojengwa na serikali ili kuongeza thamani na kurahisha upatikanaji wake.
Akizungumza katika uzinduzi wa vifungashio vya asali uliofadhiliwa na wakala wa misitu Tanzania(TFS)leo katika kijiji cha Issuna A wilayani humo Mtaturu amesema serikali iliwekeza kwa makusudi katika jengo hilo ili kuwainua wazalishaji wa asali lakini ni zaidi ya miaka mitatu sasa toka likamilike na halijaanza kutumika.
“Kauli mbiu yetu ni asali bora, maisha bora na hii inaenda sambamba na mikakati ya serikali katika kuboresha maisha ya wananchi na dira ya maendeleo ya Taifa 2025 lakini pia inaunga mkono Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 iliyoahidi kuendeleza program ya ufugaji nyuki ili kuwajengea uwezo wadau,”alisema Mtaturu.
Aliwapongeza TFS kwa juhudi zao katika uhifadhi wa misitu na kutoa mafunzo kwa kamati za mazingira karibu vijiji vyote wilayani humo  lakini pia kwa hatua yao ya kuleta vifungashio na kwa wadau kuendelea na ushirikiano waliouonyesha.


Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na  kaimu meneja wa TFS wilaya Samson Lyimo zinaonyesha kuwa  kila mwaka uzalishji wa asali unaongezeka ambapo mwaka  2014/2015 ilikuwa  tani 3.6 na 2015/2016 tani 4.617 na kusisitiza kufuatwa kwa kanuni za kuwa na mizinga bora,uvunaji bora na kutumia vifungashio vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ambapo ameeleza changamoto waliyokuwa wanaipata ya kushindwa kuwafikia wafanyabiashara kutokana na kutokuwa na eneo maalum.

 Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akionyesha moja ya kifungashio bora cha asali katika uzinduzi wa vifungashio hivyo. 

 Mkurugenzi wa wilaya ya Ikungi  Rustika Turuka akitoa salam kwenye uzinduzi  wa vifungashio vya asali uliofanyika katika kijiji cha Issuna wilayani humo.


Wafanyabiashara na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo wakimsikiliza mgeni rasmi kwa umakini.

No comments

Powered by Blogger.