Header Ads

Nishati ya uhakika inahitajika kwa ukuaji wa uchumi – Prof. Muhongo



Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiongoza kikao  kilichoshirikisha watendaji kutoka  kampuni zinazojishughulisha na  utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi za Statoil na ExxonMobil pamoja na  Wizara ya Nishati na Madini na  Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC)
MH2 
Meneja Mkazi wa Kampuni  inayojishughulisha na  shughuli za   utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta  ya  Statoil Tanzania, Øystein Michelsen, (kushoto) akielezea shughuli zakampuni  hiyo kwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia)
MH3 
Meneja Mkazi wa Kampuni  inayojishughulisha na  shughuli za   utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta  ya  Statoil Tanzania, Øystein Michelsen akisisitiza jambo  katika kikao hicho.
MH4 
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (mbele) akiongoza kikao  kilichoshirikisha watendaji kutoka kampuni zinazojishughulisha na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na  gesi za  British  Gas (BG),  Ophir, Pavilion pamoja na  Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo  ya  Petroli Nchini (TPDC)

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa   ili  Tanzania  iweze kuwa nchi ya  viwanda, nishati ya uhakika inahitajika  na kutaka makampuni kuwekeza katika uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi.
Profesa Muhongo aliyasema hayo jijini  Dar es  Salaam   katika  nyakati  tofauti alipokutana na  watendaji wa kampuni zinazojishughulisha na  Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi  pamoja na wataalam kutoka  Wizara ya Nishati na Madini na  Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) lengo likiwa ni  kupokea taarifa ya maendeleo ya miradi mbalimbali  ya makampuni hayo.
Kampuni hizo zinazofanya  kazi kwa kushirikiana na  Shirika la TPDC  ni pamoja na  British  Gas (BG),  Ophir,  ExxonMobil na Statoil.
Profesa Muhongo alisema kuwa hakuna nchi yoyote  duniani iliyopiga hatua kimaendeleo bila kuwa na nishati ya uhakika ya  umeme na kuwataka  wawekezaji kuchangamkia  fursa kupitia  gesi nyingi iliyogunduliwa.
Alitaja maeneo yanayohitaji uwekezaji   katika kuzalisha  umeme kwa kutumia gesi  kuwa ni pamoja na Mtwara,  Lindi, Somanga Fungu, na Mkuranga
Aliongeza kuwa   viwanda  37 pamoja na  vya sementi  vinahitaji  gesi na kusisitiza kuwa  iwapo sekta ya  gesi itatumiwa ipasavyo inaweza kuchangia nchi  kupiga hatua na kuingia katika  kundi la nchi zenye kipato cha  kati ifikapo mwaka 2025 kama  Dira ya Maendeleo  ya Taifa inavyosema.
Wakati huo huo Profesa Muhongo, aliwataka watendaji kutoka  Wizara ya Nishati na Madini  na  Taasisi zake kufanya kazi kwa kasi ili kuendana na kasi ya uwekezaji katika  shughuli za utafutaji na uchimbaji  wa gesi na mafuta.
“Sekta ya gesi na mafuta ambayo ni mpya inahitaji umakini  na kasi  ili kuvutia wawekezaji  zaidi,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Akizungumzia   mikakati ya serikali katika kuzalisha  wataalam  katika masuala ya mafuta na gesi Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imekuwa ikitoa ufadhili kwa wanafunzi katika ngazi  za shahada za uzamili na uzamivu katika  vyuo  vilivyopo nje ya nchi  vyenye uzoefu katika  fani hiyo, pamoja na uanzishwaji wa programu hizo katika   Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha  Dodoma (UDOM) na  Chuo  cha Madini.
Alisema kuwa  mpaka sasa kuna idadi ya takribani wanafunzi 98 waliohitimu masomo hayo  na kuziomba kampuni hizo   kuajiri wataalam hao  ili wawe na mchango mkubwa kwenye  sekta ya gesi.
“ Nia ya Serikali ni kuwa na wataalam wazawa ambao  watanufaika  kupitia  uchumi  wa gesi kwa kufanya kazi katika  viwanda vya kuchakata gesi na kuzalisha umeme unaotokana na  gesi,” alisema Profesa Muhongo.
Naye   Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) Dk.  James Mataragio alisema kuwa  shirika  hilo  limekuwa likishirikiana na  kampuni hizo katika  hatua zote muhimu hususan katika kiwanda cha  kuchakata  gesi asilia  kimiminika (Liquefied Natural Gas) na  kuongeza kuwa mpaka sasa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda limeshapatikana.
Alisema kuwa,   Tanzania inatarajia kuwa kitovu kikuu cha gesi barani  Afrika kwani  gesi nyingi  itakayozalishwa  itauzwa katika nchi nyingine.
Aliongeza kuwa nchi kama  Uganda,  Jamhuri ya  Demokrasia  ya Kongo na  Zambia  zimeonesha nia ya  kuhitaji  gesi kwa ajili ya kuzalisha nishati ya uhakika kwa kuwa nchi hizo  zinatumia maji kuzalisha umeme ambapo uzalishaji wake  hupungua hususan  wakati wa kiangazi kutokana na kupungua kwa kina  cha maji.
Naye Meneja Mkazi wa Kampuni  ya  Statoil Tanzania, Øystein Michelsen, alisema kuwa kampuni yake  ipo  tayari kushirikiana na Serikali  kuhakikisha kuwa miradi yake inakamilika kwa wakati.
Alisema  tangu  kampuni hiyo kuanza  shughuli zake nchini,  imekuwa ikishirikiana na  Serikali kwa kutoa ufadhili wa masomo  katika masuala ya  gesi na mafuta nje ya nchi kwa wanafunzi wanaofanya  vizuri.
Aliongeza kuwa kampuni ya  Statoil imekuwa ikitoa elimu ya  ujasiriliamali kwa wakazi wa mkoa wa Mtwara  ili waweze kushiriki  katika uchumi wa gesi kupitia  utoaji wa  huduma  zake kwa Kampuni hiyo.

No comments

Powered by Blogger.