Header Ads

Mgodi wa dhahabu wa MMG GOLD Ltd kuannza Uzalishajji Septemba, 2016

Na Teresia Mhagama

Imeelezwa kuwa mgodi wa kati wa dhahabu uliopo katika kijiji cha Seka wilayani Musoma utaanza uzalishaji mwezi Septemba mwaka huu.

Hayo yameelezwa wilayani Musoma wakati wa Ziara ya Waziri wa Nishati na Madini,  Profesa Sospeter  Muhongo aliyoifanya katika mgodi huo ili kukagua uendelezaji wa mgodi husika.

Akiwa katika mgodi huo alielezwa kuwa ujenzi wa  mitambo itakayotumika    kuzalisha dhahabu unaendelea vizuri na umefikia asilimia 95.

Awali, mgodi huo ulipaswa kukamilika  Juni 30,  2016 lakini umechelewa  kutokana na changamoto mbalimbali  kama kutokamilika kwa   vibali vya ujenzi wa Eneo
la kutupia mabaki ya dhahabu, upatikanaji wa mkandarasi wa kuleta kemikali za uchenjuaji (sayanaidi) na  miundombinu ya umeme Ndani ya Mgodi.


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akikagua mgodi wa Kati wa dhahabu wa MMG Gold Ltd, uliopo katika kijiji cha Seka wilayani Musoma  unaotarajia kuanza uzalishaji mwezi Septemba mwaka huu. Kushoto kwake ni Diwani wa Kata ya Nyamrandirira, Obadia  Maregesi na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma  Vijijini, Charles Magoma.
Ujenzi wa mitambo ya uzalishaji dhahabu katika kijiji cha Seka wilayani Musoma ukiendelea. Mgodi huo wa Kati wa dhahabu uliotembelewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) unatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi Septemba mwaka huu.
Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa na wanafunzi wa shule ya  msingi Bukumi, ambapo  alikabidhi madawati 71 na kumaliza tatizo la madawati katika shule hiyo.
Watendaji  mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA),Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mgodi wa dhahabu wa MMG Gold Ltd wakitazama mitambo itakayotumika kuzalisha dhahabu katika Mgodi wa Kati wa dhahabu unaomilikiwa na MMG Gold Ltd. Wa Tatu kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na wa kwanza kulia ni Kamishna Msaidizi wa Madini kanda ya Ziwa Victoria Magharibi Mhandisi Juma Sementa.

Ujenzi huo unaenda kwa kasi baada ya  Profesa Muhongo kutoa agizo kwa kampuni hiyo wakati wa ziara yake iliyofanyika  mwezi Machi Mwaka huu, kuwa ihakikishe inaanza uzalishaji dhahabu ifikapo Tarehe 30 Juni, 2016 vinginevyo itafutiwa leseni ya uchimbaji na kupewa Mtu mwingine kwani leseni hiyo ni ya muda mrefu lakini ilikuwa ikisuasua katika uendelezaji.

Aidha, Kamishna Msaidizi wa Madini kanda ya Ziwa Victoria Magharibi Mhandisi Juma Sementa,  alisema  kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Mgodi huo na hivyo ametuma ombi kwa Waziri wa Nishati na Madini kuridhia ombi la kampuni hiyo kusogeza mbele Tarehe ya kuandaa kazi ya kuzalisha dhahabu baada ya kujiridhisha na ukaguzi alioufanya mwanzoni mwa mwezi Juni, 2016.

“Mimi naridhika na maendeleo ya ujenzi yanavyokwenda,  kwa kasi hii natumaini wataweza kumaliza kazi  ifikapo Septemba 15  mwaka huu”.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Seka, Kanunu Ruhumbika, alisema kuwa ujenzi wa mgodi huo unaenda vizuri na kwamba  mgodi husika unashirikiana vizuri na wananchi kwani tayari umeanza kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi kama usambazaji wa maji na huduma ya  usafirishaji mchanga kwa ajili ya ujenzi.

“ Mara baada ya mgodi huu kuanza kazi tunategemea kufaidika zaidi kwani wameshatuahidi ujenzi wa zahanati, nyumba ya mganga, ujenzi wa shule ya Sekondari, na barabara,” alisema Ruhumbika.

Akiwa wilayani humo katika Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Muhongo pia  alikabidhi madawati katika Shule tatu za msingi zenye upungufu wa madawati ambapo katika shule ya  msingi Bukumi,  alikabidhi madawati 71 na kumaliza tatizo la madawati katika shule husika.

Akiwa katika shule hiyo pia  alifanya harambee ya uchangiaji wa mabati na saruji  kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa chumba cha darasa na nyumba ya mwalimu na yeye binafsi alitoa  mabati 100, mifuko ya saruji 100 na  Gari la kubeba vifaa vya ujenzi.

Aidha katika shule ya Msingi Kwibara A, alikabidhi madawati 36 na shule ya Msingi Kwibara B alitoa madawati 61 huku katika shule ya msingi Nyasurura, akitoa madawati 75 na hivyo kumaliza kabisa tatizo la madawati katika shule hiyo.

Akiwa katika Shule ya Msingi Nyasurura pia, aliendesha Harambee ya uchangiaji mabati na mifuko ya saruji ambapo wadau mbalimbali waliahidi kuchangia  mifuko ya saruji 9 na bati 32 huku yeye binasfi akiahidi mabati 100 na mifuko ya saruji  100.

Mpaka sasa madawati 1812  yameshachukuliwa kutoka kiwandani na kusambazwa jimboni humo huku mengine yakiendelea kutengenezwa na kusambazwa  ambapo Thamani ya dawati moja ni shilingi 83,000.

Aidha, kuhusu maji jimboni humo alisema kuwa jumla ya shilingi bilioni 1.2 imetengwa kwa ajili ya miradi ya maji ambapo ujenzi wa visima na malambo utaongezeka.

Kuhusu barabara alisema kuwa, barabara ya kutoka Musoma mjini hadi kijiji cha Busekera itajengwa kwa kiwango cha lami kwa kutumia Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/ 17.

Aidha  Profesa Muhongo aliwaagiza viongozi mbalimbali jimboni humo kuhakikisha kwamba wanajenga maktaba ili wanafunzi waweze kujisomea na kupata uelewa zaidi  hasa katika  masomo ya Sayansi na Kingereza.


Vilevile Profesa Muhongo alitoa maagizo  kwa watendaji wa Halmashauri ya Musoma Vijijini kuhakikisha wanafanya kazi ya kuwahudumia wananchi kwa kasi na atakayekwamisha juhudi za Serikali kuwahudumia wananchi atawajibishwa  “Mkurugenzi na watendaji wako, msifanye kazi kwa mazoea, hakikisheni mnawahudumia wananchi kwa kasi kama anavyohitaji Rais wetu Magufuli, 
atakayeshindwa kwenda na kasi hiyo atupishe,”alisema Profesa Muhongo.

No comments

Powered by Blogger.