Header Ads

Rais Dkt JOHN MAGUFULI atengua Uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa SHINYANGA

Na Mwandishi Maalumu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga  Bi. Anne Kilango Malecela na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Abdul Rashid Dachi, kufuatia mkoa huo kutoa taarifa zisizo sahihi kuwa hauna watumishi hewa.

Rais Magufuli ametangaza kutengua uteuzi wa Viongozi hao wa Mkoa wa Shinyanga leo tarehe 11 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam, mara baada ya kupokea Taarifa ya Mwaka 2014/2015 ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na kupokea hundi kifani ya shilingi Bilioni 6 kutoka Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizotokana na kubana matumizi.

Dkt. Magufuli ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa kuwa Mkoa wa Shinyanga hauna watumishi hewa, aliamua kutuma timu ya ukaguzi iliyokwenda kufanya uchunguzi ambapo hadi kufikia jana tarehe 10 Aprili, 2016 imebaini kuwepo watumishi hewa 45 huku zoezi likiwa linaendelea katika wilaya mbili za Ushetu na Shinyanga Vijijini.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Taarifa ya Mwaka ya utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Kamishna Valentino Mlowola Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hundi Kifani yenye thamani ya Shilingi Bilioni Sita kutoka kwa Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson mara baada ya Taasisi ya Bunge kutekeleza kwa vitendo kauli ya kubana matumizi yasio na Tija ili fedha hizo zikanunulie madawati kwa ajili ya wanafunzi.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ameishika Taarifa ya Mwaka ya utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mara baada ya kukabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Kamishna Valentino Mlowola Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson kabla ya kukabidhiwa hundi kifani yenye thamani ya Shilingi Bilioni Sita.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza katika tukio hilo la upokeaji wa Taarifa yaUtendaji wa  TAKUKURU pamoja na upokeaji wa Hundi Kifani kutoka Taasisi ya Bunge Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akisisitiza jambo katika Hotuba yake ambayo pia alitengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ane Kilango Malecela ambaye alikubali kutoa taarifa ambazo si sahihi kuwa Mkoa wa Shinyanga hauna watumishi hewa, japo katika uhakiki uliofanyika mara baada ya taarifa hiyo kumebainika kuwa kuna zaidi ya watumishi 45 ambao ni hewa.

"Na wale wote wa Shinyanga ambao walisemekana ni zero, hakuna mtumishi hewa, walikuwa tayari wameshalipwa shilingi milioni 339.9, nimejiuliza sana, na nikajiuliza sana na kwa kweli nimejiuliza sana na kwa masikitiko makubwa, kwa nini Mkuu wa Mkoa alisema hakuna mtumishi hewa?" Amesisitiza Rais Magufuli
Rais Magufuli amesema baada ya kutengua uteuzi wake, Anne Kilango Malecela atapangiwa kazi nyingine.

Pamoja na hatua hiyo, Dkt. Magufuli ametaka wakuu wa mikoa yote wawafichue watumishi hewa wote ili waondolewe mara moja, na ameagiza timu iliyofanya uchunguzi Mkoani Shinyanga itumike kufanya uchunguzi katika mikoa mingine kwa lengo la kukomesha upotevu mkubwa wa fedha za umma.

Katikati ya Mwezi Machi, 2016 Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kusimamia zoezi la kuwaondoa watumishi hewa wote katika orodha ya malipo ya mshahara, ambapo mpaka tarehe 31 Machi, 2016 Jumla watumishi hewa 5,507 walibanika.

Kati ya shilingi Bilioni 583 ambazo serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kwa ajili kulipa mishahara, kati ya shilingi Bilioni 53 na 54 zimekuwa zikipotea kutokana na kulipa mishahara ya watumishi hewa.
Baadhi ya Viongozi wa juu wa Jeshi la Magereza pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa JKT wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliyokuwa akiyatoa Ikulu jijini Dar es Salaam. 

PICHA NA IKULU

No comments

Powered by Blogger.