Kivuko cha MAGOGONI Jijini Dar es Salaam Hukusanya Shilingi Milioni 17 kwa Siku
Na Theresia Mwami TEMESA
Kivuko cha Magogoni kinakusanya hadi jumla ya shilingi milioni 17 kwa siku za kazi kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa kutokana na kutoa huduma ya kusafirisha abiria, mizigo na magari kwa kutumia vivuko vya MV Magogoni na MV Kigamboni.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa Kivuko cha Magogoni Mhandisi Lukombe King’ombe alipokuwa akitoa taarifa ya kivuko hicho kwa Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu alipotembelea kivuko hicho hivi karibuni.
Mhandisi King’ombe aliongeza kuwa kwa sasa wanakusanya mpaka milioni 17 kwa siku za Juma na kwa siku za mwisho wa wiki yaani Jumamosi na Jumapili kiasi hupungua kidogo kutokana na abiria wengi kutotumia kivuko hicho.
Aidha Mkuu wa Kivuko cha Magogoni Mhandisi Kin’gombe alimueleza Dkt. Mgwatu kuwa hali ya makusanyo hivi sasa inaridhisha kwani abiria wengi wameanza kurudi kutumia kivuko hicho baada ya kujiridhisha kuwa MV Magogoni imerudi kutoka kwenye ukarabati mkubwa na sasa inafanya kazi vizuri.
Kwa upande wake Dkt. Mgwatu alimuagiza Mhandisi King’ombe kuhakikisha kuwa wanaziba mianya yote ya upotevu wa mapato kivukoni hapo ili kuhakikisha wanafikia lengo la kukusanya shilingi milioni 19 kwa siku ambayo ni agizo la Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Profesa Makame Mbarawa alipotembelea kivukoni hapo mapema mwezi Oktoba mwaka huu.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi TEMESA alitembelea na kukagua kivuko cha Magogoni ili kujiridhisha utendaji kazi wa kivuko hicho.
Post a Comment