YANGA, POLISI KOMBAINI KUCHEZA JUMAMOSI TAIFA.
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Timu Kombaini ya Polisi
Tanzania na Yanga, Jumamosi hii zitacheza mchezo wa kirafiki katika
uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam ili kujiweka sawa katika mashindano
yanayowakabili ambapo Yanga inajiandaa kushiriki kombe la Kagame na
Kombaini ya Polisi inajiandaa kushiriki katika michezo ya Umoja wa Wakuu
wa Majeshi ya Polisi kusini mwa Afrika (SARPCCO) itakayoanza mwishoni
mwa mwezi huu nchini Swaziland.
Akizungumza jana jijini Dar es
Salaam, Mkuu wa kitengo cha Michezo wa Jeshi la Polisi, Jonas Mahanga
amesema kikosi cha Polisi kitatumia mchezo huo kubaini mapungufu na
kuyafanyia marekebisho kabla ya kuelekea nchini Swaziland ambapo alisema
taratibu zote zimeshakamilika.
Alisema Mchezo huo utakuwa
mzuri na wa kuvutia kutokana na wachezaji wanaounda kombaini ya
Polisi kuonyesha kiwango kikubwa katika kambi yao inayoendelea katika
Chuo Cha Taaluma ya Polisi(DPA) kilichopo kurasini jijini Dar es Salaam.
Mahanga alisema kombaini ya
Polisi inaundwa na wachezaji Askari kutoka timu za Polisi za Tanzania
bara na Zanzibar ambapo wengi wa wachezaji hao ni wale waliokuwa
wanacheza ligi kuu ya bara na Zanzibar pamoja na ligi daraja kwanza.
Aidha Mahanga alisema kwa
Upande wa Timu ya Mpira wa Pete nayo itacheza mchezo wa kirafiki na
Kombaini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania ili kuhakikisha kuwa inafanya
vizuri nchini Swaziland na kurudi na ubingwa.
Alisema kwa ujumla timu zote
zinazojiandaa na michezo hiyo zinaendelea vizuri ambapo Wanariadha
waliokuwa katika kambi ya Taifa mkoani Manyara wiki hii wataungana na
wenzao ili kufanya mazoezi kwa pamoja.
Lengo la Michezo hiyo ya
SARPCCO ni kujenga mahusiano miongoni mwa Askari Polisi wa nchi za
kusini mwa Afrika pamoja na kubadilishana mbinu za kukabiliana na
uhalifu ambapo Polisi Tanzania itashiriki katika mchezo wa mpira wa
miguu, pete, riadha na vishale.
Post a Comment