Header Ads

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn Kuwasili Nchini Kesho


Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

Waziri Mkuu wa Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn anatarajiwa kuwasili nchini kesho, Machi 31 kwa ziara  ya kitaifa ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiao wa Afrika Mashariki,  Dkt. Suzan Kolimba alisema kuwa ziara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Dessalegn imetokana na mkutano kati yake na Mhe. Dkt. Magufuli uliofanyika baada ya mkutano wa kawaida wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika hivi karibuni  huko nchini Ethiopia.

Aliongeza kuwa madhumuni ya ziara hiyo ni pamoja na kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Ethiopia pamoja na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara.

Mahusiano ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri, Ethiopia imeonesha nia ya kufungua Ubalozi wake hapa nchini hivi karibuni. Kwa sasa Ethiopia inawakilishwa nchini na Balozi wake aliyepo Nairobi nchini Kenya” alisema Naibu Waziri Kolimba.
Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Dessalegn atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo, watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari.

Aprili 01 mwaka huu, Waziri mkuu huyo wa Ethiopia atatembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa Bandarini hapo. Mhe. Dessalegn na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Ethiopia.
Mwaka 2015 Waziri Mkuu wa Ethipia Mhe. Dessalegn alitembelea Tanzania na kushiriki uzinduzi wa Kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua viluwiluwi vya mbu wanaoeneza Malaria kilichojengwa Kibaha, Pwani kwa ufadhili wa Serikali ya Cuba.

No comments

Powered by Blogger.