Header Ads

Dkt MPOKI: Wanaosafiri nje ya Nchi wapatiwe Chanjo ya Homa ya Manjano

Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto-Idara Kuu ya Afya,Dkt.Mpoki Ulisubisya akikabidhiwa kitabu kipya cha kadi ya manjano na mmoja wa wauguzi wa Hospitali ya mnazi mmoja ya Jijini Dar es salaam.Katibu mkuu huyo mapema leo ametembelea kituo hicho kwa ajili ya kujionea wananchi wakipata chanjo pamoja na kubadilisha vitabu vipya vya njano hiyo ambapo mwisho wa zoezi hili ni mwezi huu.
.........................................
Wananchi wanaosafiri nje ya nchi wametakiwa kupata chanjo ya homa ya manjano pale wanapohitaji kusafiri hususan siku kumi kabla ya kusafiri na kupatiwa vitabu vipya.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu,Wizara ya afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati alipotembelea hospitali ya Mnazi Mmoja jijini hapa kwa ajili ya kujionea utaratibu wa kutoa chanjo pamoja na kubadilisha vitabu vipya vya chanjo hiyo kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam.
“chanjo hii ni muhimu hasa kwa zile nchi zenye changamoto za homa hii ya manjano,kwahiyo ni vizuri kuwa na kinga kabla ya kusafiri nchi hizo ili usije pata ugonjwa huo,’nilikua nchi ya Angola hivi karibu watu karibu elfu mbili walipoteza Maisha”amesema Dkt.Mpoki
Hata hivyo kutokana na wingi wa watu kwa jiji la Dar es salaam na uhitaji wa chanjo hiyo wamekubaliana kuweka taratibu ya kupunguza watu kupoteza muda wa kufika mnazi mmoja kupata chanjo hiyo,hivyo wameamua kupeleka huduma hiyo karibu na wananchi mahali walipo
“Muda ambao upo huku shughuli nyingi zinasimama,hivyo wataalam watakaa na kuona mahali gani panafaa ili watu msipoteze muda wakuja hadi huku mfano wa Ubungo wapate huko huko hivyo tunazitawanya huduma hizi sehemu mbalimbali kwenye vituo vyetu vya huduma za afya na taratibu zitatolewa”.
Kuhusu vitabu vipya vya chanjo Dkt. Mpoki amesema wanavyo vya kutosha hivyo hamna haja ya wananchi kuwa na wasiwasi kama watakosa vitabu kwani hakuna siku itatokea watanzania wote wakasafiri kwa siku mmoja,na hivyo utaratibu mpya utatenganisha wale watu wa kuchanja na wakubadilisha vitabu wasikae sehemu moja
Akijibu maswali ya wananchi waliofika kupata chanjo hiyo pamoja na kubadilisha vitabu Kaimu Mkurugenzi wa Kinga toka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt.Khalid Massa alisema,kwa wale watanzania watakaotaka kuchanja watapatiwa vitabu vipya kwa kulipia shilingi elfu ishirini ila kwa wale ambao watahitaji kubadilisha kadi  peke yake watalipia kiasi cha shilingi elfu tano.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mnazi Moja Dkt. Sophinia Ngonyani amesema chanjo hii ya manjano ni muhimu sana kwani zinazuia maambukizi ya ugonjwa wa manjano hususan kwa Watanzania wanaosafiri kwenda nchi zenye ugonjwa huo.
Ametaja tangu zoezi hili lianze la kubadilisha vitabu vipya na chanjo ya kudumu. Hospitali  yake inachanja watu wapatao 100 hadi 150 wa siku na  kwa wale wanaofika kubadilisha vitabu vipya wanapokea watu wapatao 200 kwa siku na kuongeza kuwa wanavyo vitabu vya kutosha.
Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kupita kwa Waziri wake Mhe.Ummy Mwalimu mnamo mwezi Novemba mwaka jana alizindua vitabu vipya ya homa ya manjano ikiwa na lengo la kudhibiti utolewaji holela wa kadi hizo na kwenye taarifa yake kwa Umma ya mwezi februari mwaka huu aliwahimiza wananchi wajitokeze kubadilisha vitabu hivyo ambapo mwisho wa kubadilisha itakua ni tarehe 31 machi mwaka huu,hivyo kuanzia tarehe Mosi Aprili kadi za zamani hazitatambulika tena.Zoezi la kubadilisha vitabu hivi lilianza tarehe 9 Januari ,2017.
Nchi zilizoainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa na hatari za maambukizi ya ugonjwa wa homa ya manjano nchi 30 za Bara la Afrika  ambazo ni Angola, Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameron, Afrika ya Kati, Chad, Congo,   Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Equatorial Guinea, Ethiopia, Gabon, Gambia, Ghana, Guinea, Ginea Bissau, Kenya, Liberia, Mali, Mauritania, Niger, Nigeria, Rwanda, Senegal, Sierra Leone,  Sudan ya Kusini,  Sudan, Togo na Uganda
Aidha,nchi 13 kutoka Bara la Amerika ya Kusini ambazo ni  Argentina, Bolivia, Brazil, Colombia, Ecuador, French Guiana, Guyana, Panama, Paraguay, Peru, Suriname, Trinidad na Venezuela.

Dkt.Mpoki akiongea na wananchi waliofika kwenye kituo hicho kwa ajili ya kupata chanjo ya homa ya manjano.


Katibu Mkuu Dkt. Mpoki akiwaonesha kitabu kipya cha homa ya manjano ambacho inambidi mwananchi anayesafiri toka nchini Tanzania na kwenye nchi thelathini za Bara la Afrika anatakiwa awe amepata chanjo hiyo ili kumkinga na maambukizi ya homa ya manjano.Kitabu hicho(kadi) ni mbadala ya kile cha zamani ambapo kipo tofauti na ina lenga kudhibiti udanganyifu wa raia kupata kitabu bila kupata chanjo.

No comments

Powered by Blogger.