Header Ads

CCM yaridhia Mabadiliko ya Katiba, yaweka Historia Ndani ya Ukumbi wa Kikwete, DODOMA

Mwenyekiti  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais John Magufuli, amesema mabadiliko na mageuzi yanayoanza kufanyika ndani ya chama hicho, yamalenga kuhakikisha ccm inaenda kwa wananchi na sio kwa viongozi.

 Aidha amesema marekebisho hayo ya katiba ambayo yamelenga kuboresha mfumo na muundo wa ccm, ni muhimu kufanyika kwani utendaji wa ccm kwa kuwa umekua ukishuka kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Pia ametoa wito kwa wana ccm kuhakikisha katika uchaguzi ndani chama hicho unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao, wanachagua viongozi wenye uwezo wa kazi na sio fedha, na pia wasichague watu mapandikizi.

 Rais magufuli amesema hayo alipokua akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano mkuu maalumu mjini hapa leo Machi 12.2017,kwenye ukumbi mpya wa CCM  Dodoma, ambao amependekeza uitwe ukumbi wa Kikwete (Kikwete Hall) jina ambalo wajumbe wa mkutano huo waliridhia kwa kauli moja.

 Maeneo ambayo amesema ni lazima yafanyiwe mabadiliko ni kupunguza idadi ya vikao, wajumbe wa vikao, vyeo, na kwamba umefika wakati kwa viongozi kwenda kwa wananchi.

 Amefafanua kuwa mabadiliko hayo pia yamelenga kuijenga kiuwezo ccm isiwe omba omba hasa wakati wa uchaguzi mkuu.

Rais magufuli amewatoa hofu wana CCM kwamba mabadiliko hayo ndani ya chama ni ya kawaida kulingana na mazingira na mahitaji na amewaomba wajumbe wa mkutano mkuu maalumu waunge mkono mabadiliko hayo ya katiba.


Katibu wa CCM Taifa ndugu Abdulrahman Kinana akizungumza kwenye mkutano huo.

 Wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)kwa kauli moja wamepitisha mabadiliko ya Katiba na kanuni za chama na jumuiya zake.

 Mabadiliko hayo yanalenga kutoa maboresho kwenye Muundo, Uongozi na Mfumo lengo likiwa ni kuleta mageuzi ndani ya chama.

Akizungumza katika mkutano huo maalum Katibu wa CCM Taifa ndugu Abdulrahman Kinana amesema mageuzi hayo hayamlengi mtu wala kikundi chochote bali yanalenga kutoa ufanisi ndani ya Chama.

 Amesema CCM imekuwa na utamaduni wa mabadiliko na imeshafanya hivyo mara 15 na awamu hii ni mara ya 16 sasa dhamira ikiwa ni kuweka uhai,ubora na ushindi wa CCM.

Ametaja mabadiliko waliyoyalenga kuwa ni kupunguza utitiri wa vyeo,idadi ya vikao ambavyo wakati mwingine vinakosa ajenda na kuamua kubaki kushughulikiana na imepunguza idadi ya wajumbe.

Ndugu Kinana amefananisha mabadiliko hayo na vyama vingine vikongwe duniani ikiwemo chama cha African National Congress(ANC)cha nchini Afrika Kusini na chama cha Kikomunist cha China ambacho kina wanachama wengi lakini idadi ya wajumbe wa mikutano yao wakiwa wachache.

Mkutano huo mkuu maalum umehudhuriwa na 2,356 kati ya wajumbe wa 2,380 sawa na asilimia 99.78.

Baadhi ya wajumbe wakiwa katika mkutano huo.

Kikwete alonga:

Mwenyekiti  mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dokta Jakaya Kikwete amesema hatua ya Chama hicho kufanya mabadiliko kwenye katiba yake,sio dalili ya udhaifu bali ni kujiimarisha.

Dokta Kikwete amesema hayo Leo alipokua akiwasalimu wana CCM waliohudhuria mkutano Mkuu maalum wa CCM leo  mjini Dodoma.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliolenga kufanya mabadiliko kadhaa ya katiba ya Chama hicho amesema  mabadiliko hayo sio dalili ya udhaifu bali ni kujiimarisha.

Naye makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dokta Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa viongozi wa CCM  wakiwemo wajumbe wa mkutano huo kujenga mazoea ya kuipitia katiba na kanuni za chama hicho na pia wazingatie maadili.

Wakati huo huo CCM imepokea wanachama wapya watatu ambao walikuwa wafuasi wa vyama vya upinzani ambao ni makamu mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) bara Said Arfi, aliyekuwa mbunge Kasulu mjini Moses Machali na mjumbe wa kamati Kuu ya CHADEMA dokta Yared Furuso ambapo wamesema kilichowavutia kuhamia CCM ni utendaji kazi wa rais dokta Magufuli.

Awali wakati wa kusoma Hotuba yake,  Dk. Magufuli amesema serikali yake itaendelea kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya, kuwatumbua watumishi wabadhirifu na kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya usafiri na umeme.

Amesema moja ya malengo makubwa ya serikali yake ni kuhakikisha Taifa la Tanzania linakua salama kwa kupiga vita biashara ya dawa za kulevya, kulinda mipaka ya nchi, muungano na kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na maji.

Hata hivyo amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake, changamoto kubwa ambayo imeendelea kuwepo ni umasikini, ukosefu wa ajira, uwajibikaji usioridhisha na migogoro ya wakulima na wafugaji.

Kufuatia changamoto hizo amesema eneo ambalo linaweza kutoa ajira kwa watanzania wengi ni viwanda na kusema hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha Tanzania inafikia azma ya nchi ya viwanda na kufafanua mpaka sasa viwanda 2169 vimesajiliwa ikiwemo viwanda vya mbolea, chuma na usindikaji mazao.

Amesema lengo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020, sekta ya viwanda ichangie asilimia 40 ya ajira zinazozalishwa nchini.

Katika hatua ya mwisho, Mkutano huo umepitisha mabadiliko ya nafasi tatu ndani ya CCM  ikiwemo nafasi ya Katibu wa NEC Uchumi na Fedha ambayo kwa sasa itaongozwa na Dokta Frank Haule. 

 Nafasi hiyo awali ilikuwa chini ya mama Zakiah Meghi.

 Akitoa mapendekezo hayo yaliyopitishwa na wajumbe wote wa mkutano huo mwenyekiti wa CCM Taifa dokta John Magufuli amemtaja ndugu Abdallah Juma Abdallah kuwa naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.

 Awali nafasi hiyo ilikuwa ikiongozwa na ndugu Vuai Ally Vuai.

Nafasi nyingine ni nafasi ya katibu wa NEC Organizesheni ambapo kwa sasa itakuwa chini ya ndugu Pereira Ame Silima ambapo awali ilikuwa chini ya dokta Seif Khatibu.

Amewatakia kila la kheri viongozi waliokuwepo katika nafasi na kuahidi kutowasahau.

Shuhudia picha za mkutano mkuu hapa:

       
Baadhi ya sehemu ya mabalozi na wawakilishi wa Mabalozi wa nchi mbalimbali hapa nchini wakifuatlia mkutano huo.

   
Msanii wa Bongo Movie Aunty Ezekiel akiwa katika mkutano huo .

 
Vijana wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam.

Wajumbe wakibadilishana mawazo mara baada ya kumalizika kwa mkutano Mkuu maalum wa CCM.

   
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose Bhanji akiwa pamoja na Mbunge wa Viti maalum Bi. Oliva Semgeruka mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

  
Mbunge wa Nzega Mjini akisalimiana na wajumbe wenzake wa mkutano huo mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

  
Sehemu ya wanahabari wakiendelea kuchukua habari wakati mkutano huo ukiendelea.

Mwandishi wa Clouds  Tv, Salum Mwinyimkuu akiwa pamoja na Mwandishi Mwandamizi wa Mtandao wa MO Blog, Andrew Chale.

No comments

Powered by Blogger.