Header Ads

TAHADHARI: Hedifoni Zalipuka Mwanamke akisikiliza Muziki kwenye Ndege Australia

Maafisa wa serikali nchini Australia wametahadharisha watu dhidi ya kutumia vifaa vinavyotumia betri wanaposafiri kwenye ndege.
Hii ni baada ya headphone (Hedifoni/kifaa cha kusikilizia sauti kwenye simu na mitambo mingine ya kompyuta) zilizokuwa zinatumiwa na abiria mmoja kulipuka.
Mwanamke huyo alikuwa amelala akiwa kwenye ndege iliyokuwa safarini kutoka Beijing hadi Melbourne pale alipozinduliwa na mlipuko mkubwa.
Alizitoa hedifoni hizo, ambazo hutumia betri, upesi kutoka kichwani na akagundua zilikuwa zinatoa cheche za moto.
Zilishika moto na kuanza kuyeyuka.

Wahudumu walikimbia na kumsaidia kuzima moto huo kwa kumwagilia hedifoni hizo maji kwa kutumia ndoo.
Kufikia wakati huo, betri ya hedifoni hizo pamoja na kifuniko chake cha plastiki vilikuwa vimeyeyuka na kukwamilia sakafuni.
"Kwa sehemu iliyosalia ya safari, abiria walilazimika kuvumilia harufu kali ya plastiki zilizokuwa zimeyeyuka, vipande vya hedifoni hiyo zilivyokuwa vimeungua na nywele za mwanamke huyo ambazo zilichomeka pia," ATSB walisema kupitia ripoti baadaye.
Ripoti hiyo haikusema hedifoni hizo zilikuwa za muundo gani lakini inaaminika kwamba huenda mlipuko huo ulisababishwa na kasoro kwenye betri za lithium-ion zinazotumiwa katika hedifoni hizo.

No comments

Powered by Blogger.