Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi
wa Mtwara katika siku ya mwisho wa ziara yake katika Viwanja vya Mashujaa mkoani
Mtwara. .............................
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 05 Machi, 2017
amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 4 katika mikoa ya Pwani, Lindi na
Mtwara.
Kabla ya kuondoka
Mjini Mtwara na kurejea Jijini Dar es Salaam Mhe. Rais Magufuli amefanya
mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mjini Mtwara ambapo amesema
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha inasukuma maendeleo ya Mtwara
na Lindi kwa nguvu kubwa kwa manufaa ya wananchi.
Amesema Serikali
imedhamiria kutilia mkazo juhudi za uendelezaji wa bandari ya Mtwara, ujenzi wa
barabara, uimarishaji wa miundombinu ya nishati ya umeme, ujenzi wa viwanda
vikubwa na usimamizi mzuri wa shughuli za kilimo ambavyo vitasaidia kukuza
uchumi, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu.
Mhe. Rais Magufuli
amewapongeza viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa mafanikio
yaliyopatikana katika soko la korosho lililopita na ameagiza wale wote
waliohusika kufuja fedha za wakulima wachukuliwe hatua.
Aidha, Mhe. Dkt.
Magufuli amesema Tanzania itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake mzuri na
nchi jirani ya Msumbiji na ametaka suala la wahamiaji haramu wanaoondolewa
nchini humo wakiwemo Watanzania lisikuzwe huku akisisitiza kuwa Serikali
haiwezi kuwatetea watu wanaishi katika nchi nyingine bila kufuata sheria.
Kuhusu Mkoa wa
Mtwara kufanya vibaya kielimu, Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Mtwara
kubadilika kwani juhudi za Serikali kuwapelekea maendeleo hazitakuwa na maana
kama wananchi watakuwa hawana elimu.
"Nimeambiwa
hapa watu wanapenda sana disco na ngoma, watoto badala ya kusoma wanacheza
disco, hapo tunakwenda pabaya" amesisitiza Mhe.
Rais Magufuli.
Mkutano wa Mhe.
Rais Magufuli Mjini Mtwara umedhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Nishati na
Madini Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.
Makame Mbarawa, Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Philip Mpango, Wabunge na
viongozi wa taasisi.
|
Post a Comment