Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amewaagiza viongozi wa Serikali
kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi mkoani Singida kuwabaini
na kuwachukulia hatua za kisheria wananchi wanaohujumu miundombinu ya barabara
na kuisababishia hasara Serikali.
Profesa Mbarara ametoa
agizo hilo mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya
yenye urefu wa Kilomita 89.3 kwa kiwango cha lami na kubaini kuwa baaadhi ya
wananchi wameanza kuhujumu barabara hiyo.
“Tumepanga kujenga
barabara ya Mkiwa-Itigi-Makongolosi kwa kiwango cha lami, sasa kitendo cha
kuanza kuhujumu barabara iliyokwisha kamilika ni kitendo kisichokubalika na
hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesisitiza
umuhimu wa kila mwananchi wa Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla kuilinda
miundombinu ya barabara, reli na mawasiliano ambayo inajengwa kwa fedha nyingi
ili idumu kwa muda mrefu.
“Tutaimarisha stesheni
ya Itigi na kuimarisha mawasiliano ya simu ili kuwezesha eneo hili kuwa na
mawasiliano ya uhakika na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Singida”,
amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
|
Post a Comment