Ripoti: Ushindi wa Trump ni hatari kwa dunia
Trump anaongoza miongoni mwa wagombea wa Republican
Shirika moja la kimataifa limesema ushindi wa Donald
Trump unachukuliwa kuwa miongoni mwa hatari 10 kuu zaidi zinazokabili dunia.
Shirika hilo la Economist Intelligence Unit linaonya kuwa
iwapo Bw Trump atashinda urais Marekani, hilo huenda likavuruga uchumi wa dunia
na kuongeza hatari za kisiasa na kiusalama dhidi ya Marekani.
Hata hivyo, shirika hilo halimtarajii Bw Trump,
anayeongoza kwenye kinyang’anyiro cha kumchagua atakayepeperusha bendera ya
chama cha Republican, kumshinda Bi Hillary Clinton ambaye shirika hilo linasema
"ana uwezekano mkubwa sana kuwa mgombea wa chama cha Democratic".
Ushindi wa Trump unaorodheshwa kuwa hatari zaidi kwa
dunia kushinda hata Uingereza kuondoka kutoka kwa Umoja wa Ulaya au hata
makabiliano ya kivita katika bahari ya South China Sea.
Kuyumba kwa uchumi wa Uchina au Urusi kuingilia kivita
Ukraine na Syria na kusababisha “vita baridi” vipya ni miongoni mwa mambo
ambayo yanachukuliwa kuwa hatari zaidi ya ushindi wa Bw Trump.
"Kufikia sasa, Bw Trump ametoa maelezo machache sana
kuhusu sera zake, na huwa anabadilisha sana msimamo wake,” EIU wanasema kwenye
ripoti yao ya utathmini wa hatari zinazokabili dunia.
Utathmini huo huangazia pia athari za jambo fulani na
uwezekano wa jambo hilo kutokea.
EIU hutumia kipimo cha moja hadi 25, na Bw Trump ana
alama 12, sawa na hatari ya "kuongezeka kwa ugaidi wa kijihadi kuathiri
uchumi wa dunia”.
"Amekuwa na msimamo mkali sana dhidi ya biashara
huria, pamoja na Nafta, na ameituhumu Uchina mara nyingi kuwa taifa
linalofanyia mchezo sarafu,” EIU inasema.
Shirika hilo limeonya kuwa matamshi yake makali dhidi ya
Mexico na Uchina hasa yanaweza kusababisha vita vya kibiashara.
Bw Trump amependekeza ua ujengwe kati ya Marekani na
Mexico kuzuia wahamiaji na pia ametetea kuuawa kwa jamaa za magaidi. Aidha,
amependekeza kuvamiwa kwa Syria ili kuangamiza kundi la Islamic State.
EIU wanasema pendekezo msimamo wake kuhusu mzozo
Mashariki ya Kati pamoja na pendekezo kwamba Waislamu wazuiwe kuingia Marekani
vinaweza kutumiwa na makundi ya itikadi kali za Kiislamu kuwatafuta wafuasi
zaidi.
Post a Comment