Na. Veronica
Kazimoto
OFISI ya Taifa ya Takwimu imekabidhiwa magari tisa aina ya Land cruiser yenye thamani ya Dola za
kimarekani laki nne na elfu tano ($ 405,000) sawa na Shillingi za kitanzania Milioni
mia nane na kumi (810,000,000/=) kutoka Shirika lisilo la kiserikali la ICAP
linaloendeshwa na Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani kwa ajili ya Utafiti
wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika mwezi Septemba, 2016.
Akizungumza katika
hafla ya kukabidhiana magari hayo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amelishukuru
Shirika la ICAP kwa msaada huo ambao utasaidia kupunguza gharama za kukodi
magari kwa ajili ya kufanyia utafiti.
“Napenda kuchukua fursa
hii kulishukuru Shirika la ICAP kwa kutupatia msaada huu wa magari tisa yenye
thamani ya Shillingi milioni mia nane na kumi. Huu sio msaada mdogo kwani fedha
ambazo zingetumika kukodisha magari ya utafiti, sasa zitatumika katika shughuli
nyingine za kimaendeleo,” amesema Dkt. Chuwa.
Amesema katika
kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), takwimu rasmi zinahitajika ili
kupima utekelezaji wake na hivyo utafiti huu utakapokamilika utasaidia kutoa
takwimu zitakazotumika kupima utekelezaji wa malengo hayo.
|
Mkurugenzi Mkuu wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza leo jijini Dar es
Salaam katika hafla ya kukabidhiana magari tisa yenye thamani ya Shillingi
Millioni mia nane na kumi kutoka Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili ya Utafiti
wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia
mwezi Septemba, 2016. Kushoto kwake ni Claud Kumalija mwakilishi wa katibu Mkuu
wa Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
|
|
Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS),
Dkt. Fatuma Mrisho akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya kukabidhiana
magari tisa
yenye thamani ya Shillingi Millioni mia nane na kumi kati
ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili ya Utafiti
wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia
mwezi Septemba, 2016. Kushoto kwake ni Claud Kumalija mwakilishi wa katibu Mkuu
wa Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kulia kwake ni
Dkt. Michelle Roland Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti
Magonjwa – (Centre for Disease Control and Prevention - CDC).
|
|
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika wa Taasisi ya Marekani
ya Kudhibiti Magonjwa – (Centre for Disease Control and Prevention - CDC) Dkt.
Michelle Roland akikata utepe kuashiria kukabidhi rasmi magari tisa yenye
thamani ya Shillingi Millioni mia nane na kumi kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika
nchi nzima kuanzia mwezi Septemba, 2016.
|
|
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt.
Albina Chuwa akiwasha gari kama ishara ya kupokea magari tisa yenye thamani ya
Shillingi Millioni mia nane na kumi kutoka Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili
ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima
kuanzia mwezi Septemba, 2016. Hafla ya makabidhiano ya magari hayo imefanyika
leo jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mkaazi wa Shirika la ICAP Tanzania, Dkt. Fernando Morales amesema utafiti huu
unalenga kupima Viashiria na Matokeo ya UKIMWI nchini ili kujua ni kwa kiwango
gani Tanzania imepiga hatua katika kupambana na ugonjwa huo.
Dkt. Morales amesema
msaada huu wa magari utasaidia kurahisisha usafiri wa kutoka eneo moja la
utafiti hadi lingine na kuweza kusaidia katika upatikanaji wa taarifa muhimu za
utafiti huu.
Nae Mkurugenzi Mkaazi
wa Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Magonjwa – (Centre for Disease Control and
Prevention - CDC) Dkt. Michelle Roland amesema kutokana na utafiti huu
kufanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ukusanyaji wa takwimu, kutasaidia
kupunguza gharama ambazo zingetumika kama utafiti huu ungefanyika kwa njia ya
kutumia madodoso ya karatasi.
Ameongeza kuwa utafiti
huu utafanyika kwa kutumia sampuli wakilishi ya kaya zipatazo 15,800 Tanzania
Bara na Tanzania Zanzibar, na kuwafikia walengwa wapatao elfu arobaini (40,000)
wakiwemo watoto wasiopungua elfu nane (8,000).
Matokeo yanayotarajiwa
kupatikana katika utafiti huo ni pamoja na taarifa sahihi kuhusu hali ya
maambukizi mapya ya VVU, upatikanaji wa huduma za tiba na matunzo kwa watu
wanaoishi na VVU hapa nchini na kutambua ni kwa kiwango gani huduma hizi
zimesaidia katika kuudhibiti ugonjwa wa UKIMWI.
Utafiti huu wa
Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utafanywa kwa pamoja na Shirika la ICAP
Tanzania, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa
Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya
Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).
|
Post a Comment