Watendaji
mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa
Madini Tanzania (TMAA),Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mgodi wa dhahabu
wa MMG Gold Ltd wakitazama mitambo itakayotumika kuzalisha dhahabu katika Mgodi
wa Kati wa dhahabu unaomilikiwa na MMG Gold Ltd. Wa Tatu kushoto ni Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na wa kwanza kulia ni Kamishna
Msaidizi wa Madini kanda ya Ziwa Victoria Magharibi Mhandisi Juma Sementa.
Ujenzi huo unaenda kwa kasi baada ya Profesa
Muhongo kutoa agizo kwa kampuni hiyo wakati wa ziara yake iliyofanyika
mwezi Machi Mwaka huu, kuwa ihakikishe inaanza uzalishaji dhahabu ifikapo
Tarehe 30 Juni, 2016 vinginevyo itafutiwa leseni ya uchimbaji na kupewa Mtu
mwingine kwani leseni hiyo ni ya muda mrefu lakini ilikuwa ikisuasua katika
uendelezaji.
Aidha, Kamishna Msaidizi wa Madini kanda ya Ziwa
Victoria Magharibi Mhandisi Juma Sementa, alisema kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Mgodi
huo na hivyo ametuma ombi kwa Waziri wa Nishati na Madini kuridhia ombi la
kampuni hiyo kusogeza mbele Tarehe ya kuandaa kazi ya kuzalisha dhahabu baada
ya kujiridhisha na ukaguzi alioufanya mwanzoni mwa mwezi Juni, 2016.
“Mimi naridhika na maendeleo ya ujenzi
yanavyokwenda, kwa kasi hii natumaini wataweza
kumaliza kazi ifikapo Septemba 15 mwaka huu”.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Seka, Kanunu Ruhumbika,
alisema kuwa ujenzi wa mgodi huo unaenda vizuri na kwamba mgodi husika unashirikiana vizuri na wananchi
kwani tayari umeanza kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi kama usambazaji wa
maji na huduma ya usafirishaji mchanga
kwa ajili ya ujenzi.
“ Mara baada ya mgodi huu kuanza kazi tunategemea
kufaidika zaidi kwani wameshatuahidi ujenzi wa zahanati, nyumba ya mganga,
ujenzi wa shule ya Sekondari, na barabara,” alisema Ruhumbika.
Akiwa wilayani humo katika Jimbo la Musoma Vijijini,
Profesa Muhongo pia alikabidhi madawati katika
Shule tatu za msingi zenye upungufu wa madawati ambapo katika shule ya
msingi Bukumi, alikabidhi madawati 71 na kumaliza tatizo la madawati
katika shule husika.
Akiwa katika shule hiyo pia alifanya harambee ya
uchangiaji wa mabati na saruji kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa chumba
cha darasa na nyumba ya mwalimu na yeye binafsi alitoa mabati 100, mifuko ya saruji 100 na Gari la kubeba vifaa vya ujenzi.
Aidha katika shule ya Msingi Kwibara A, alikabidhi
madawati 36 na shule ya Msingi Kwibara B alitoa madawati 61 huku katika shule
ya msingi Nyasurura, akitoa madawati 75 na hivyo kumaliza kabisa tatizo la
madawati katika shule hiyo.
Akiwa katika Shule ya Msingi Nyasurura pia, aliendesha
Harambee ya uchangiaji mabati na mifuko ya saruji ambapo wadau mbalimbali
waliahidi kuchangia mifuko ya saruji 9 na bati 32 huku yeye binasfi
akiahidi mabati 100 na mifuko ya saruji 100.
Mpaka sasa madawati 1812 yameshachukuliwa kutoka
kiwandani na kusambazwa jimboni humo huku mengine yakiendelea kutengenezwa na
kusambazwa ambapo Thamani ya dawati moja ni shilingi 83,000.
Aidha, kuhusu maji jimboni humo alisema kuwa jumla ya
shilingi bilioni 1.2 imetengwa kwa ajili ya miradi ya maji ambapo ujenzi wa
visima na malambo utaongezeka.
Kuhusu barabara alisema kuwa, barabara ya kutoka
Musoma mjini hadi kijiji cha Busekera itajengwa kwa kiwango cha lami kwa
kutumia Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/ 17.
Aidha Profesa Muhongo aliwaagiza viongozi
mbalimbali jimboni humo kuhakikisha kwamba wanajenga maktaba ili wanafunzi
waweze kujisomea na kupata uelewa zaidi hasa katika masomo ya Sayansi na Kingereza.
Vilevile Profesa Muhongo alitoa maagizo kwa
watendaji wa Halmashauri ya Musoma Vijijini kuhakikisha wanafanya kazi ya
kuwahudumia wananchi kwa kasi na atakayekwamisha juhudi za Serikali kuwahudumia
wananchi atawajibishwa “Mkurugenzi na
watendaji wako, msifanye kazi kwa mazoea, hakikisheni mnawahudumia wananchi kwa
kasi kama anavyohitaji Rais wetu Magufuli,
atakayeshindwa kwenda na kasi hiyo atupishe,”alisema Profesa Muhongo.
|
Post a Comment