Watanzania Waaswa Kufanya Usafi wa Mazingira kwa Hiari ya Shuruti
Na.Aron Msigwa-MAELEZO
Wito umetolewa kwa Taasisi,mashirika, makampuni na watu binafsi kuanzia ngazi ya familia kuendelea kuitumia Siku ya jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kufanya usafi wa mazingira, kupanda miti na kutunza vyanzo vya maji kwa hiari bila kusubiri kushurutishwa na sheria kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wakiwemo wafanyabiashara na wafanyakazi wa taasisi na mashirika mbalimbali waliokuwa wakitekeleza wakifanya usafi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam leo wamesema kuwa hatua ya Serikali kuirasimisha Siku ya jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kuwa siku ya usafi wa mazingira kitaifa inaweka msisitizo kuhusu jukumu la kila mwananchi kuwa mlinzi na mwangalizi wa mazingira katika sehemu anayoishi.
Wamesema Suala la usafi wa mazingira linawahusu watu wote, hivyo kila mwananchi anao wajibu wa kushiriki kikamilifu kufanya Usafi wa Mazingira kwenye Makazi yake, Maeneo ya Biashara, maeneo ya Taasisi za Umma na maeneo yenye mikusanyiko ya watu mbalimbali kama masoko na minada.
Bi. Zaituni Musa mkazi wa Mwananyamala, Kinondoni jijini Dar es salaam aliyekuwa akisafisha mifereji eneo la mtaa anaoishi akishirikiana na wananchi wenzake amesema kuwa suala la usafi wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi bila kuangalia cheo au nafasi yake katika jamii kwa kuwa kuishi katika mazingira machafu kuna athari kubwa kiafya hususan kuchangia milipuko ya magonjwa ikiwemo Kipindupindu.
" Suala la usafi wa mazingira linatuhusu sote, ni wakati wa kuchukua hatua na kuacha kuishi kwa mazoea,nawaomba watanzania wenzangu tufanye usafi bila kulazimishwa na Serikali kila mmoja atimize wajibu wake" Amesisitiza Bi.Zaituni.
Baadhi ya Wakazi wa Mwananyamala wakipakia Taka walizozoa katika mitaa yao katika gari la kuzoa Taka la Manispaa ya Kinondoni. |
Nao baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka eneo la Mwananyamala na wale wa Soko la vyakula la Buguruni, Manispaa ya Ilala waliokuwa wamefunga maduka na biashara zao kupisha muda wa kufanya usafi wa mazingira kuanzia saa 12 hadi saa 4 asubuhi wamesema kuwa uamuzi wa Serikali kuitangaza Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kuwa Siku ya Usafi wa mazingira unatoa fursa kwao Kufanya Usafi wa mazingira katika maeneo wanayofanyia biashara tofauti na awali.
" Watanzania wote wa Mijini na Vijijini tujenge desturi ya kuweka mazingira yetu katika hali ya usafi wakati wote na katika jambo hili kila mmoja wetu awe mlinzi wa kukemea watu wenye tabia za kutupa taka hovyo ili maeneo yetu yawe katika hali ya usafi na yakuvutia wakati wote" Amesisitiza Bw. Haule John mmoja wa wafanyabiashara hao.
Aidha, wamesisitiza kuwa ili kuyaweka maeneo mbalimbali katika hali ya usafi Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 lazima itumike kwa mtu yeyote atakayekaidi kufanya usafi siku hiyo kutozwa faini isiyopungua shilingi elfu hamsini au kifungo cha kuanzia miezi mitatu mpaka miaka saba, faini ya shilingi laki mbili ya papo hapo na shilingi milioni tano kwa kampuni au taasisi itakayotupa taka hovyo atatozwa.
Ikumbukwe kuwa Desemba 23 mwaka jana, Serikali kupitia kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Luhaga Mpina ilitangaza kuwa usafi wa mazingira nchi nzima utakuwa ukifanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Mhe.Mpina alisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya viongozi na watendaji wanaopuuzia kusimamia shughuli za usafi katika siku hiyo pia kwa wananchi wanaoshindwa kufanya usafi katika maeneo yao kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake pamoja na Sheria ndogo.
Aidha, kabla ya jumamosi ya kila mwezi kutangazwa kuwa siku ya Usafi nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kuzingatia sheria ya Sikukuu za Kitaifa, aliamua maadhimisho ya sherehe za Uhuru , 9 Desemba 2015 kwa upande wa Tanzania Bara yatumike kufanya usafi wa mazingira nchi nzima na kuhamasisha watu kujituma kufanya kazi.
Post a Comment