Makamu wa Rais SAMIA SULUHU Mgeni Rasmi Futari ya Watoto June 26
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Mama Samia Hassan Suluhu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio la futari maalum iliyoandaliwa kwa watoto waishio Mazingira magumu na hatarishi tukio litakalofanyika Juni 26.2016 ndani ya viwanja vya shule ya Sekondari ya Wavulana ya Azania, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wanahabari mapema leo Juni 21.2016, Mkurugenzi wa kampuni ya Nisha’s Film Production, Bi. Salma Jabu “Nisha” ameeleza kuwa, tayari maandalizi yote yamekamilika na tukio hilo maalum litafanyika katika viwanja hivyo vya shule ya Azania ambapo Makamu huyo wa Rais pamoja na viongozi wengine watahudhuria pia wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mbunge wa Ilala, Idd Hassan Zungu pamoja na viongozi wa dini na wageni wengine waalikwa.
Akielezea suala hilo, Nisha amebainisha kuwa, akiwa kama msanii na ambaye ni kioo cha jamii na pia ni balozi wa kituo cha watoto waishio katika mazingira magumu cha New Hope Family kilichopo Kibada Mwasonga-Dar es Salaam, hivyo kwa tukio hilo ni moja ya kurudisha fadhira kwa jamii pamoja na kuweza kukutana nao kwa pamoja.
“Wito kwa dini yetu ya kiislamu hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu tunapaswa kutoa Dhaka pamoja na kuonyesha upendo kwa wenzetu wanaoishi katika mazingira magumu hasa watoto Yatima, Walemavu, wanaoishi mitaani pamoja na watoto wenye ulemavu wa ngozi kwa kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali ambazo zinaweza kuwa sehemu ya faraja kwao” alieleza Nisha.
Tazama tukio hilo Hapa:
Meneja wa Nisha Film Production, Bwana Myovela Mfuasi akizungumza na wanahabari (Hawapo pichani) wakati wa tukio hilo la kampuni yao hiyo juu ya kufuturisha watoto waishio katika mazingira magumu itakalofanyika Juni 26.2016 katika shule ya sekondari ya Azania.
Afisa Habari wa kampuni ya Nisha Film Production, Baraka Nyaganda, wa pili kutoka kushoto, akizungumza katika tukio hilo anayemfuatia ni Meneja wa kampuni hiyo, Bi. Salma Jabu 'Nisha' na wa kwanza kulia ni mmoja wa watoto wanaopatiwa misaada, Mtoto Lazaki Rashid.
Mkurugenzi wa kampuni ya Nisha Film Production, Bi. Salma Jabu 'Nisha' akipitia taarifa hiyo kwa wanahabari.
Mkutano huo ukiendelea..
Mkurugenzi wa kampuni ya Nisha Film Production, Bi. Salma Jabu 'Nisha' akisoma taarifa hiyo kwa wanahabari (Hawapo pichani).
Mkurugenzi wa kampuni ya Nisha Film Production, Bi. Salma Jabu 'Nisha' akizungumza na wanahabari (Hawapo pichani) wakati wa tukio hilo.
Futari hiyo inatarajiwa kufanyika siku ya Jumapili Juni 26.2016 katika uwanja huo wa shule ya sekondari Azania ambapo tiukio hilo linatarajia kuanza majira ra saa 10 jioni na litaendelea hadi saa mbili usiku.
Watoto na watu wote waishio pembezoni mwa jiji la Dar e Salaam wanatarajiwa kufikiwa ambapo pia viongozi na wasimamizi wa vituo vilivyopo Jijini Dar es Salaam wameombwa kufahamishwa tukio hilo kwa ushiriki wao ambapo pia wanaweza kuwasiliana kupitia namba 0676894246 ama 0789586057.
Aidha, Nisha akijibu swali la mwanahabari wa mtandao huu juu ya kama yupo tayari kutengeneza filamu inayoelezea watoto waishio katika mazingira magumu, ambapo ameeleza kuwa tayari amesha andaa filamu hiyo na ndani ya miezi miwili hadi mitatu inatarajia kuingia sokoni.
“Kwa sasa tayari nimesha andaa filamu inayozungumzia mazingira ya watoto waishio mazingira magumu na pia ndani ya filamu hii, Msanii Joti ameweza kushiriki pia” alijibu Nisha.
Aidha, baadhi ya filamu zake ni pamoja na Mtaa kwa Mtaa, Macho yangu, Kashfa, Gumzo, Zena na Betina na zingine nyingi.
Post a Comment