Mhandisi HAMAD MASAUNI akabidhi Vifaa vya Michezo
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni ambae pia ni Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amekabidhi vifaa vya
michezo ikiwemo jezi na mipira kwa manahodha wa timu kumi zinazotarajiwa kushiriki mashindano yaliyopewa
jina la Masauni - Jazeera CUP 2016, katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika
katika ofisi ya Jimbo la Kikwajuni.
Akizungumza kabla ya kutoa vifaa hivyo vya michezo,
Mhandisi Masauni alisema lengo la kuanzisha ligi hiyo ni kuwafanya vijana wawe
na afya pamoja na kujiepusha kuwa katika magenge mabaya ambayo yanaweza
kusababisha kijana kushawishiwa kujiingiza katika matendo ya uhalifu huku ikiwa ni moja ya ahadi
aliyohaidi wakati wa kipindi cha kampeni kuboresha michezo katika jimbo hilo.
Nahodha wa timu ya Kikwajuni Bondeni, Salum Said
(kushoto), akipokea jezi kutoka kwa
Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni ambae pia ni Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mhandisi Hamad Masauni(kulia).
|
Muonekane wa nyuma wa moja ya jezi zitakazotumiwa
katika mashindano ya kombe la Masauni/Jazeera , kutoka maeneo mbalimbali katika Jimbo la Kikwajuni
kama inavyoonekana.
|
“Vijana ni nguvu kazi ya Taifa lolote lile duniani
linalotaka kupiga hatua katika sekta ya maendeleo, lengo la mashindano haya
yanayoenda kuanza leo ni kuwaepusha vijana kujiingiza au kushawishiwa kushiriki
matendo ya uhalifu ikiwa pamoja na kulinda afya zao,” alisema Masauni.
Mmoja wa manahodha wa timu zilizokabidhiwa vifaa
hivyo, Salum Said alisema wanawashukuru wadhamini wa kombe hilo ambao ni Mbunge
wa Kikwajuni, Mhandisi Hamad Masauni na Mwakilishi wa Jimbo hilo Nassor Salim
Jazeera kwa kutambua uwepo wa vijana huku akiahidi timu yake ya Kikwajuni
Bondeni kuwa bingwa wa ligi hiyo.
Mashindano hayo yatatanguliwa na mchezo wa kirafiki
utakaowakutanisha timu ya Maveterani wa Jimbo la Kikwajuni na Kundi la G1.
Post a Comment