Mgodi wa Dhahabu wa Geita wakabidhi Vifaa vya Watoto Hospitali ya Muhimbili
Na Neema Mwangomo
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imepokea msaada wa vifaa mbalimbali vya watoto vyenye thamani ya Shilingi Milioni 23 kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Msaada huo umetolewa kupitia chama cha Madaktari wa watoto Tanzania.
Vifaa vilivyotolewa ni BP Machine 10, Infusion Pump 2, Thermometers 110, Standing Weighing Scales 6, Lying Down Weighing Scales 6, Nebulies 3 pamoja na Pulse Oxymeter 10.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa GGM, Terry Mulpeter, Daktari Mkuu wa mgodi wa GGM, Kiva Mvungi amesema lengo ni kuwa sehemu ya jamii, lakini pia kutambua juhudi zinazofanywa na madaktari wa watoto katika kuboresha huduma za afya.
“GGM kama mdau katika sekta ya afya imeamua kutoa msaada huu ili watoto na kina mama watakaofika Muhimbili waweze kupata huduma hizi muhimu kwani tunatambua changamoto mnazopata katika kuwahudumia watoto, lakini pia tunatambua mchango wenu,” amesema Daktari Mvungi.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Tiba MNH ambaye ni Mkuu wa Idara ya Watoto, Daktari Mary Charles amesema msaada huo umekuja wakati muafaka kwani vifaa hivi ni muhimu na vinahitajika kwa ajili ya kuwahudumia watoto .
“Tunawashukuru GGM kwa msaada wenu ni vifaa muhimu sana kwani unapotaka kumpatia dawa mtoto hauangalii umri bali unaangalia uzito wake hivyo unampima uzito kwanza alafu unampatia dawa kulingana na uzito wake” Amesema Dk. Charles.
Kwa mujibu wa Dk Charles jengo la watoto hulaza watoto 300 ambapo pia kila kliniki ina uwezo wa kuchukua watoto 60.
Post a Comment