Header Ads

Watanzania washauriwa Kujifunza Mchezo wa YOGA

Na Raymond Mushumbusi,WHUSM


Watanzania wameaswa kujifunza mchezo wa Yoga ili kuimarisha miili yao na kujikinga dhidi ya matatizo mengi yanayosababishwa na mfumo wa maisha.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye mara baada ya kushiriki katika mahadhimisho ya  Siku ya Kimataifa ya Yoga yaliyofanyika katika viwanja vya Coco.

Mhe. Nape Nnauye alisema kuwa mchezo huo unatoa fursa kwa watu wa kabila, dini na mataifa mbalimbali kujumuika pamoja na kujifunza utamaduni na michezo mbalimbali.

“ Yoga sio kwa jamii ya kihindi peke yake ila ni kwa ajili ya watu wote Duniani na nawashauri watanzania wenzangu tujifunze mchezo huu kwa manufaa ya afya zetu na maendeleo ya michezo nchini”.Alisema Mhe. Nnauye.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akifanya mazoezi mbalimbali katika kuadhimisha Siku ya kimataifa ya Yoga iliyofanyika Leo June 19, 2016 Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Balozi wa India nchini Mhe. Sandip Arya ameshukuru Serikali kupitia Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kutoa ushirikiano mkubwa  katika kufanikisha Siku ya kimataifa ya Yoga na kuahidi kuendelea kushirikiana zaidi katika kuendeleza michezo nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Mchezo wa  Kabaddi ambao ni wasimamizi wa mchezo wa Yoga nchini Bw. Abdallah Nyoni amesema Siku ya kimataifa ya Yoga ni fursa kwa watanzania kujifunza mchezo huo hasa vijana ili kujenga uwezo kwa watanzania kushiriki katika michezo mbalimbali ikiwa ni juhudi za kuendeleza michezo na na kuongeza ajira nchini.

Yoga ni mazoezi ya kiroho na kimwili yenye asili katika falsafa ya Uhindi, hujumuisha umoja wa roho na mwili, mawazo na matendo na uelewa kati ya mwanadamu na mazingira yanayomzunguka pamoja na mtazamo wa kuijumla wa afya ya binadamu.

Desemba 11,2014,Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha mapendekezo na kukubali azimio ambalo lilitambua Juni 21 kila mwaka iwe siku ya Kimataifa ya Yoga kwa kusambaza taarifa zaidi kuhusu faidi za Yoga duniani.

No comments

Powered by Blogger.