Serikali Kukomesha Mtandao Unaosafirisha Binadamu
SERIKALI imejipanga kukomesha
mtandao wa watu wasiowaaminifu ambao wanajihusisha na biashara ya
kusafirisha binadamu kwenda nchi mbalimbali duniani.
Mtandao huo unahusisha raia wa
Tanzania waliopo ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na raia wa kigeni
kutoka nchi za India, Malaysia, nchi za Falme za Kiarabu na Mashariki
ya Kati.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Bi. Mindi Kasiga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam.
“Serikali kwa kushirikiana na
Jumuiya ya Watanzania wanaoishi katika nchi za Bara la Asia pamoja na
baadhi ya wahanga wa biashara hiyo inashughulikia kupata majina ya
wahusika wote, ikiwemo walioko kwenye Balozi ambao wanawezesha
upatikanaji wa visa kuwakamata na kuwafikisha katika mkono wa sheria”
alisema Mindi.
Ili kukomesha mtandao huo,
Serikali imeanda utaratibu maalumu kwa wafanyakazi wanaokwenda katika
nchi za ukanda huo ikiwa ni pamoja na kuandaa mikataba kulingana sheria
za nchi husika.
Mindi amesema kuwa kwa nchi ya
Omani tangu mwezi Machi 2011 hadi Septemba 2015, Serikali kupitia
Ubalozi imeratibu ajira za Watanzania 4358 ambapo kati ya hizo ajira
4033 ni za watumishi wa majumbani.
Aliongeza kuwa, kwa upande wa
nchi za Mashariki ya Kati, kuanzia mwezi Juni, 2015 Serikali ilikataza
rasmi Watanzania kwenda kufanyakazi zisizo na ujuzi au za ndani katika
nchi hizo hadi hapo ilipopata ufumbuzi wa changangamoto zilizokuwa
zikisababishwa na mtandao uliokuwa unajihusisha na usafirishaji wa
binadamu.
Aidha, ili kuwasaidia Watanzania
kupata fursa za ajira nje ya nchi, Serikali inaendelea na jitihada za
kusaini mikataba ya Ushirikiano na nchi hizo ikiwemo mkataba wa Tanzania
na Qatar.
Mtandao huo wa kusafirisha
binadamu umekua ukitoa ahadi za ajira kwa wasichana wenye umri wa kati
ya miaka 18 na 24, kwa kuwalaghai kuwa na fursa za ajira katika
mahoteli, migahawa, maduka makubwa au kazi za nyumbani, kitu ambacho si
ukweli.
Hata hivyo, wengi wa Watanzania
wanaoenda nje ya nchi kwa kusaidiwa na mtandao huo wamekuwa wakipata
matatizo kadhaa, ikiwemo mateso, mikataba yao kukiukwa, kulazimishwa
kufanya ukahaba, na hatimaye kukimbilia Ubalozini ili kupatiwa misaada
mbalimbali.
Aidha, imedhihirika kuwa
Watanzania walio katika nchi za Bara la Asia, Falme za Kiarabu na
Mashariki ya Kati wamekuwa wakiomba misaada ya kurudishwa nchini kupitia
Balozi hizo wakiwemo watanzania 500 waliopo nchini India.
Post a Comment