Serikali yaahidi Kuwatia Mbaroni Wahusika wa Mauaji ya Watafiti Mkoani Dodoma
Na Beatrice Lyimo-
MAELEZO
SERIKALI
imesema itahakikisha kuwa wahusika wa mauaji ya Watafiti mkoani Dodoma
wanakamatwa na kufikishwa mahakamani ili waweze kujibu mashtaka yanayowakabili.
Kauli hiyo imetolewa
leo jijini Dar es salaam na Waziri ya Mambo ya
Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa mkutano na waandishi wa habari juu ya mauaji ya Wataalamu
hao yaliyotokea wilayani Chamwino.
Amesema kuwa Serikali
imesikitishwa na hatua iliyochukuliwa na
baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Iringa Mvumi wilayani Chamwino kuwaua
watafiti hao ambao walikuwa kazini.
Kufuatia hali hiyo amewaagiza
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kushirikiana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI)
katika kufanya upelelezi wa mauaji ya wataalamu hao ili wahusika waweze kufikishwa vyombo vya
usalama haraka na haki iweze kutendeka.
Amesema kuwa
ushirikiano huo utasaidia kuimarisha upepelezi
ambao utawezesha uandaaji wa mashtaka ili wahusika wote waweze kufikishwa
Mahakamani kwa ajili ya kujibu mashtaka yanayowakabili.
“Wizara inawataka
Mkurugenzi wa Mashtaka DPP ajihusishe kikamilifu na upelelezi wa kesi hii ya mauaji ya watafiti kwa kushirikiana na
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai DCI kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya
Uendeshaji wa Mashtaka” alifafanua Dkt.
Mwakyembe.
Ameongeza kuwa ili
kukomesha wimbi la wananchi kuchukua sheria mkononi, Wizara itachukua hatua kali
kuhakikisha waliohusika kwa namna moja ama nyingine kwa kushawishi, kuhamasisha
au kuchochea, kupanga, kushambulia kwa mapanga na kushiriki kuchoma moto gari
wanafikishwa mahakamani ili Sheria ichukue mkondo wake.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mwakyembe amewataka baadhi ya waandishi wa habari kubadilisha
mfumo wa kutoa taarifa za matukio zinazochochea uvunjifu wa amani kama vile
kuandika kuwa “wananchi wenye hasira kali” maneno ya aina hii hushawishi wengine
kufanya hivyo kwa kisingizio cha hasira.
Mbali na hayo Waziri
huyo amevitaka vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa wote waliohusika
na vitendo vya kuchukua sheria mkononi ikiwemo kuwafikisha mahakamani.
Post a Comment