Header Ads

Wadau wa Habari Washindwa Kuusoma Muswada, Kamati ya Bunge yatoa siku 7

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya  Jamii Mhe. Peter Serukamba(katikati) pamoja na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye(kushoto)  na Naibu Sppika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson wakiwasiliza baadhi ya wadau wa habari (hawapo pichani) wakitoa maoni yao kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 katika kikao kilichofanyika leo Oktoba 19,2016 Mjini Dodoma.

Licha ya kupewa zaidi ya mwezi mmoja tangu Bunge lilipoweka hadharani Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari, wadau mbalimbali wa Habari wameshindwa kuwasilisha maoni yao kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kwa madai ya kutousoma na hivyo kulazimika kupewa siku saba zaidi.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Peter Serukamba alipokuwa akitoa marejesho kwa Waandishi wa Habari mara baada ya kukutana na wadau mbalimbali wa habari nchini kujadili na kupata maoni kutoka kwa wadau hao kuhusu muswada huo.

“Niwapa wadau wiki moja wawe wameleta maoni yao kwa maandishi yaani mpaka Jumatano ya wiki ijayo wawe wameyawasilisha kwa Kamati kwa kuwa leo tumewaita wakasema hawakupata muda wa kusoma,” alisisitiza Mhe. Serukamba.

Mhe. Serukamba ameongeza kuwa mchakato wa kuunda sheria unashirikisha wadau husika kwa kuleta maoni yao juu ya Mswada husika na maoni yao yanasaidia katika kutengeneza sheria iliyo nzuri kwa ajili ya Tasnia ya Habari na maendeleo yake kwa ujumla.

Ameeleza kusikitishwa na wadau hao kushindwa kusoma muswada huo au kuonekana wana ajenda yao na kusisitiza kuwa anaamini kwa muda ambao Kamati imetoa kwa wadau kuwasilisha maoni yao kwa kamati watakuwa wamewasilisha maoni kwa wakati ila kamati iyapitie kabla ya kupelekwa kwa Spika wa Bunge na kuanza kujadiliwa Bungeni.

Miongoni mwa wadau waliofika lakini wakashindwa kuwasilisha maoni ni Jukwaa la Wahariri, Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MoAT), Chama cha Wanasheria Nchini na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini.

Licha ya wadau hao kudai muda ulikuwa mdogo, muswada huo ulichapishwa kwenye tovuti ya Bunge katikati mwa Septemba mwaka huu huku Waziri wa Habari, Nape Nnauye akifanya mkutano na wanahabari Septemba, 16, akiuarifu umma kutoa maoni yao.

Kabla ya muswada huo kuwasilishwa Bungeni, Serikali ilishirikisha wadau katika mchakato wa ndani na walitoa maoni yao.

Katika barua ya Machi 31 mwaka huu, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, akiwakilisha maoni ya taasisi zaidi ya 10 ikiwemo TEF, MCT, LHRC,Citizen’s Information Bureua, walitoa maoni yao ikiwemo kupendekeza jina la muswada.

“Zaidi ya asilimia 90 ya muswada huu ni maoni ya wadau wa habari na tunayo kwa maandishi,” alisema Waziri Nape akiijulisha Kamati jana mjini Dodoma kuwa kwa upande wa Serikali wadau walishashirikishwa na sasa imebaki hatua ya kanuni za Bunge.

No comments

Powered by Blogger.