Header Ads

Serikali yawataka Wadau wa Tasnia ya Habari Kutoa Maoni Kuhusu Muswada wa Habari

Na Beatrice Lyimo

SERIKALI imevitaka wadau wa vyombo vya habari nchini kuacha kulalamika na badala yake waendelee kutoa maoni yao kuhusu muswada wa sheria kwa vyombo vya habari ambao unatarajiwa kuwasilishwaa katika Bunge lijalo mjini Dodoma.

Akizungumza katika wakati tofauti wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi za Vyombo vya habari nchini, Mkurugenzi wa Idara ya  Habari(MAELEZO), Hassan Abbas alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa muswada huo unapitishwa na Bunge ili uweze kuwa sheria kamili na hatimaye kuifanya tansia ya habari kuzidi kuheshimika.

Mkurugenzi Abbas alisema tangu muswada huo uliposomwa kwa mara ya kwanza Bungeni, mwezi Septemba mwaka huu,  wadau wa tasnia ya habari nchini ikiwemo Wahariri na waandishi wa habari wamekuwa mstari wa mbele kupingana katika mitandao ya kijamii badala ya kutoa maoni yao katika mamlaka zinazohusika.

“Ni aibu kwa maoni ya muswada huu yanayohusu tasnia ya habari kutolewa na watu ambao hawana taaluma ya habari, hivyo tukiwa kama wanataaluma ni vyema tujitokeze kwa wingi kutoa maoni kifungu kwa kifungu ili kuweza kuboresha muswada” alisema  Mkurugenzi Abbas.

Aliongeza kuwa haitopendeza kwa muswada huo kuendelea kutolewa maoni na wananchi wengine na wadau wa muswada kukacha kutoa maoni yao, na hivyo kusababisha muswada huo kuandikwa na watu walio nje ya tasnia ya habari.

Abbas alisema, muswada huo utakusudia kuiongezea nguvu tasnia ya habari kwa kuweka ikiwemo suala zima la kuzingatia sheria na mipaka ya nchi katika utoaji wa habari na taarifa maalum za Serikali kwa umma kwa kuzingatia ukomo wa kimataifa.

“Azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948, pamoja na kuzungumzia kuhusu haki ya kupata taarifa lakini pia limeanisha sheria mbalimbali ambazo hazina budi kuheshimiwa, na sheria hizo ni pamoja na sheria za ulinzi na usalama” alifafanua Mkurugenzi Abbas.

Akifafanua zaidi alisema taaluma ya habari ni tasnia muhimu katika maendeleo ya taifa ila kwa upande mwingine inaweza kuharibu maendeleo kwa njia moja au nyingine na hivyo kuwataka wadau wa habari kujitokeza kutoa maoni kwa kujenga hoja za msingi ili kuboresha muswada badala ya kulalamika.

Aidha kwa upande  mwingine, Abbas alisema Ofisi yake ni mlezi na mratibu wa vyombo vya habari na hawana budi kuwasiliana naye pindi wanapopata changamoto mbalimbali ikiwemo utoaji na upatikanaji wa taarifa za Serikali katika Wizara, Taasisi, Idara, Mikoa na halmashauri nchini.

Pia alisema zipo taarifa ambazo zinahitaji kufanyiwa uhakiki ikiwemo ufundi na takwimu, na hivyo aliwataka waandishi wa habari kuwa wavumilivu pale wanapohitaji taarifa hizo kutoka kwa maafisa habari wa Wizara au Taasisi husika.

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Majira, Imma Mbughuni alisema chombo hicho kimejipanga kutoa maoni yao kuhusu muswada huo na mara baada ya kumaliza wanatarajia kuwasilisha katika kamati ya kudumu ya Bunge.

Naye Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jambo Leo, Anicetus Mwesa alisema chombo chao pia kimekusudia kuupitia muswada huo ili kutoa maoni yao na baadae kuyawasilisha katika kamati husika..

                                                                                                                                                                                                                  

No comments

Powered by Blogger.