Header Ads

Rais Dkt MAGUFULI aondoka Nchini Kuelekea Kenya Kwa Ziara ya Kikazi ya Siku Mbili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akisindikizwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa tayari kwa safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili leo Oktoba 31, 2016.
..................

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John PombeMagufuli, leo tarehe 31 Oktoba, 2016 ameondoka nchini kuelekea Nairobi nchini Kenya kwa ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini humo kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Rais Magufuli ameagwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es salaam, Paul Makonda na viongozi mbalimbali wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mara baada ya kuwasili nchini Kenya, Rais Magufuli atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, na baadae atakwenda kutoa heshima katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Mheshimiwa Rais pia anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa atakayoandaliwa na mwenyeji wake Ikulu Jijini  Nairobi.

Katika ziara hiyo Rais Magufuli anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha  Eldoville kilichopo Karen Jijini Nairobi na pia kuzindua barabara mchepuko (Southern By-pass) iliyopo Jijini humo. Barabara hiyo ni moja kati ya miradi mikubwa ya barabara nchini Kenya, inayounganisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi kwa barabara za juu na chini.


Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar Es Salaam
31Oktoba, 2016 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipungia wakati akipanda ndege kwenye  Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kwa safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili leo Oktoba 31, 2016.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi,  Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda na viongozi wengine wakipunga mikono kumuaga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli  katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati akianza  safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili leo Oktoba 31, 2016.

No comments

Powered by Blogger.