Header Ads

Wananchi Waaswa kutunza Miundombinu ya Barabara Inayojengwa kwa Ushirikiano na Wafadhili

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI  Mhandisi Mussa  Iyombe akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa barabara za Halmashauri nchini unaotekelezwa kwa ushirikiano na shirika la Maendeleo la Japan (JICA) mradi unaolenga kuwajengea uwezo wahandisi wa Halmashauri na Mikoa katika kusimamia na kukarabati barabara zilizopo katika maeneo yao kwa kushirikiana na wananchi.
Muwakilishi Mkazi wa Shirika la maendeleo la Japan (JICA) bw. Nagase Toshio akifafanua kuhusu ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Japan katika kutekeleza mradi huo unaolenga kujenga uwezo kwa wahandisi wa Halmashauri hapa nchini ili waweze kuwashirikisha wananchi katika miradi ya barabara inayotekelezwa ili waweze kujiletea maendeleo.
Kiongozi wa mradi wa Ujenzi na ukarabati wa Barabara za halmashauri hapa nchini Dkt.Tatsumi Tokunaga  akisisitiza jambo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu mradi huo unaotekelezwa katika Halmashuri za Iringa,Mufindi,Chamwino na Kondoa kwa awamu ya kwanza kwa ufadhili wa Shirika la JICA kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI  Mhandisi Mussa  Iyombe akitoa ufafanuzi kwa washiriki wa Kikao cha Siku moja kilichowashirikisha Viongozi wa Mradi huo  kutoka JICA pamoja na wahandisi wa Halmashauri ambazo mradi huo unatekelezwa ukilenga kuboresha miundo mbinu katika Halmashauri hapa nchini.

Frank Mvungi-MAELEZO

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI bw. Mussa Iyombe amewataka wananchi kutunza barabara zinazojengwa  na Serikali kwa kushirikiana na wafadhili katika Halmashauri zote hapa nchini.

Akizungumza leo Jijini Dar es salaam katika hafla fupi ya kupokea ripoti ya utekelezaji wa mradi wa Ujenzi na ukarabati wa barabara za halmashauri nchini  Iyombi amebainisha kuwa mradi huo umefadhiliwa  na  Shirika  la Maendeleo la Japan (JICA) .

“Mradi huu unatekelezwa katika Halmashauri  za Iringa,Mufindi,Chamwino na Kondoa” alisisitiza Iyombe.

Akifafanunua kuhusu utekelezaji wa mradi huo  Iyombe amebainisha kuwa  unadhamiria kujenga uwezo kwa wahandisi wa Mikoa na Halmashauri hapa nchini  ili waweze kushirikiana na wananchi katika kujenga  na kulinda miundo mbinu hiyo kwa maslahi ya Taifa.

 Aidha  Iyombi  amewata wakurugenzi wa Halmashauri  ambazo mradi huo unatekelezwa  kutunza barabara hizo ili zilete matokeo yaliyokusudiwa.

Akizungumzia ushirikiano mzuri uliopo kati ya Japan na Tanzania Iyombe amesema kuwa maeneo ambayo Tanzania imekuwa ikipata ufadhili kutoka Japan ni Sekta ya Kilimo,Viwanda,Uimarishaji wa Utawala bora.

Kwa upande wake mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) bw. Nagase Toshio amesema kuwa  Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mradi wa Ujenzi na Ukarabati wa barabara katika Halmashauri hapa nchini unatekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza imekamilika katika Halmashauri za Chamwino na Iringa na awamu ya pili imekamilika katika Halmashauri za Kondoa na Mufindi ambazo ripoti ya utekelezaji wake iliwasilishwa leo katika mkutano wa siku moja ulifanyika Jijini Dar es salaam ukilenga kufanya tathmini ya utekelezaji kabla ya kuanza kwa awamu ya tatu.

No comments

Powered by Blogger.