Mawaziri wa Afya UMMY MWALIMU na Dkt HAMIS KIGWANGALLA wafanya Ziara Hospitali ya MUHIMBILI kukagua
Mawaziri wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli wameendelea kufanya kile ambacho wananchi wanataka ikiwemo suala la kutumikia wananchi ambapo mapema leo, Februari 17, Mawaziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu na Naibu wake, Dk. Hamisi Kigwangalla wameweza kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa lengo la kukagua majengo likiwemo lile aliloagiza Rais kuwa litumike kuwa wodi ya akina mama.
Mawaziri hao wamefika Hospitali hiyo ya Taifa majira ya mchana na kisha kupokelewa na wenyeji wao akiwemo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Prof. Laurance Masaru na kisha kukagua moja ya majengo lililopo jengo la watoto ilikuona namna ya kuweza kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali hyo ya Taifa.
Mbali na kukagua majengo pia walipata kuwatembelea wagonjwa na kuwafariji ikiwemo wodi maalum ya wagonjwa wa figo, wodi ya akina mama, wodi ya watoto na upasuaji mdogo pamoja na wodi ya watoto wa ugonjwa wa moyo na ile ya watoto wa ugonjwa wa kansa.
Aidha, Waziri Ummy Mwalimu ameeleza kuwa jengo ambalo Rais ameliagiza litumike kama wodi ya akina mama, amebainisha kuwa agizo hilo wameweza kulitekeleza ndani ya siku moja na awali wamefanikiwa kulaza wagonjwa zaidi ya 40 na hadi kufikia leo wameweza kufikisha wagonjwa 53.
Hata hivyo, Waziri Ummy Mwalimu amewataka wananchi na vyombo vya habari kuwa wavumilivu kwa kipindi cha sasa kwani tayari ukarabati unaendelea kuakikisha miundombinu inawekwa sawa na ndani ya wiki moja itakuwa imekamilika.
Imeandaliwa na Andrew Chale
Tazama video ya tukio hilo hapa:
(Picha zote na Andrew Chale)
Post a Comment